Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa mwito kwa wananchi wanaostahili ambao hawajajiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Setikali za mitaa, kujitokeza kwa wingi kabla zoezi hilo kufungwa keshokutwa, Jumapili, Oktoba 20, 2024.
Amesisitiza umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, akisema ni hatua muhimu katika kuhakikisha ushiriki kwenye mchakato huo ambao ni wa kidemokrasi na haki kwa kila mwananchi anayestahili.
Balozi Dk. Nchimbi ametoa mwito huo baada ya kujiandikisha kwenye daftari la wapikura la wakazi katika mtaa wake, eneo la Kilimani, jijini Dodoma leo Oktoba 18, 2024.
Balozi Dk. Nchimbi amesema ni muhimu kila mwanchi kutimiza haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika Uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 27, mwezi ujao.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kila mwananchi kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa kila kura inahesabika na inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii, ikizingatiwa kuwa viongozi watakaochaguliwa watakuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya mitaa yao.
Balozi Nchimbi amesisitiza umuhimu makundi yote katika jamii kushiriki kikamilifu, hususan vijana na wanawake, kutambua nafasi yao ya kipekee katika mchakato huo, ikiwa pia ni sehemu muhimu kwao kujihusisha na siasa kwa lengo la kuleta maendeleo katika jamii.
Pamoja na kuwasisitiza wananchi wajiandikishe na kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, Balozi Nchimbi ameisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wenye maono na uwezo wa kuongoza na kusimamia shughuli za maendeleo kama vile elimu, afya, maji safi, na miundombinu.
Aidha, ameendelea kuwataka wananchi na wadau wote wa uchaguzi, kudumisha amani na mshikamano, kuepuka kuchochea chuki katika jamii, na kuzingatia taratibu za kisheria, ili kuhakikisha maslahi ya taifa na tija kwa wananchi, vinakuwa mbele, kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.
Balozi Dk. Nchimbi akijiandikisha kwenye daftari la wapikura la wakazi katika mtaa wake, eneo la Kilimani, jijini Dodoma leo Oktoba 18, 2024
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇