Ilala, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Edward Mpogolo, amemwelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elhuruma Mabelya, kuwasaka na kuwanasa wale wote waliokopa jumla ya sh. bilioni 17 katika Halmashauri hiyo na kushindwa kurejesha.
Amesema fedha hizo ni zilizokuwa zikitolewa kwa wajasiriamali kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa kata za Mnyamani, Vingunguti na Buguruni.
“Hizi sh.bilioni 17 halmashauri iliwakopesha watu lakini hawajarejesha mpaka sasa.Ziko katika mzunguko,”alisema.
Amemtaka mkurugenzi huyo kuangalia utaratibu wa kuwatafuta na kuwapata wahusika na kuchukua hatua.
Pia alionya vikali kama kuna viongozi walijinufaisha na fedha hizo kinyume cha utaratibu kuzirejesha kabla ya kuwaumbua.
“Walipe fedha hizi ili wengine wakope. Nimemwelekeza Mkurugenzi awatafute wahusika na wachukuliwe hatua,” amesema.
Amebainisha halmashauri hiyo imetenga zaidi ya sh.bilioni 10 kwaajili ya mikopo hiyo itakayo anza kutolewa Oktoba mwaka huu.
“Hizi fedha zipo tayari katika akaunti ya Jiji la Dar es Salaam.Nimeelekeza wajasiriamali wadogo, mama na babalishe na bodaboda wapewe kipaumbele,” ameeleza DC Mpogolo.
Amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan,kwa kuruhusu fedha hizo kuanza kutolewa na kwamba awamu hii zitatolewa kwa utaratibu mzuri kupitia benki.
Amewataka wananchi watakaopata mikopo hiyo kuto kurubuniwa na wajanja wachache kuchomekwa majina kisha kupewa mgao mdogo baada ya mkopo kutoka.
DC Mpogolo anaendelea na ziara yake ya siku 10 ya kusikiliza na kutatua kero za wanchi wiayani humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇