LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 2, 2024

TANZANIA, MSUMBIJI ZAKUBALIANA KUDUMISHA USHIRIKIANO





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wamekubaliana kukuza mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. 


Marais hao wamefikia makubaliano hayo wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika wakati wa Ziara ya Kiserikali ya Rais Nyusi hapa nchini. Ziara hii ilianza na mapokezi rasmi yaliyofanyika Ikulu.


Rais Samia na Rais Nyusi pia wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta ya miundombinu kama vile barabara, reli, uchumi wa buluu na anga ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari ya ndege ya kampuni ya Air Tanzania ya moja kwa moja hadi Msumbiji. 


Sekta ya miundombinu ni muhimu katika kuunganisha nchi hizi mbili na kuboresha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu ili kukuza biashara na uwekezaji. 


Kwa upande mwingine, Marais hao wamekubaliana kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani ili kuweza kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji baina ya nchi mbili hizo kupitia miradi ya pamoja na mikakati. 


Tanzania na Msumbiji pia zimekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kama vile Jumaiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN).


Maeneo mengine waliyokubaliana kushirikiana ni kuimarisha ulinzi na usalama katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipakani.  


Mbali na mazungumzo Marais hao pia walipata fursa ya kushuhudia utiaji wa saini wa Hati mbili za Makubaliano. Hati hizo ni katika sekta ya afya inayolenga kuanzisha ushirikiano katika kufanya utafiti, kubadilishana uzoefu na kufanya programu za pamoja za masuala ya afya.  


Hati nyingine ya Makubaliano ni baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi ya Msumbiji ya Uwekezaji na Uwezeshaji Usafirishaji nje ya Nchi inayolenga kuimarisha ushirikiano na kupanua mawanda ya biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Msumbiji.  



Sharifa B. Nyanga

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages