LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 17, 2024

RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI CHUO CHA VETA RUKWA

 


 

Picha Mbalimbali ya za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika uwekaji wa Jiwe la Msingi Chuo cha VETA Mkoa WA Rukwa.

………

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi chuo cha VETA cha Mkoa wa Rukwa kilichopo katika kijiji cha Kashai, Kata ya Momoka, wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, leo tarehe 16 Julai, 2024, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Rukwa.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe. Rais amesema kwa sasa mkoa wa Rukwa unakua kiuchumi, hasa katika eneo la miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni wakati wa vijana na jamii kwa ujumla kupata chuo cha kuwawezesha kupata ujuzi, utaalamu na maarifa ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko hayo makubwa ya kiuchumi.

“Chuo hiki ni jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba vijana na jamii yetu inatayarishwa na kupewa elimu ujuzi utakaowasaidia kujitegemea kwa kujiajiri au kuajiriwa,” amesisitiza.

Akimkaribisha Rais ili kuweka jiwe la msingi katika chuo hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka msisitizo katika ujenzi wa vyuo vya VETA kote nchini na kuhakikisha kwamba kazi kubwa waliyopewa ya kuhakikisha Watanzania wanapata mafunzo ya ufundi stadi inatekelezwa kwa ufanisi.

Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa chuo hicho cha VETA cha Mkoa wa Rukwa, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amesema ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 90% na umegharimu shilingi Bilioni 6,088,085,195.15, ukiwa na jumla ya majengo 24 ambayo ni pamoja na Jengo la utawala 1, Nyumba za watumishi 3, Karakana 8, Jengo 1 la madarasa(General Classes), kibanda cha mlinzi 1, Nyumba ya Jenereta 1, Jiko na bwalo la kulia chakula 1, Maktaba 1, Mabweni 4 na Maabara ya kumpyuta 1.

CPA Kasore ameongeza kuwa chuo hicho kilianza kutoa mafunzo rasmi tarehe 18 Machi, 2024 kwa wanafunzi 63 wa fani mbili za Mafunzo ya muda mrefu za Umeme wa majumbani yenye wanafunzi 49 na Ubunifu wa nguo, ushonaji na teknolojia ya mavazi yenye wanafunzi 14.

“Pamoja na kozi hizi mbili (2) za muda mrefu tulizokwishaanza kuzitoa, tunatarajia kuongeza kozi nyingine 7 za Uashi, Uungaji na Uundaji vyuma, Ufundi Magari, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, Upishi, Useremala na Uchakataji wa Chakula ifikapo Januari 2025,” aliongeza.

Nae Happiness Florence mwanafunzi wa fani ya Umeme wa majumbani amemshukuru Rais na Serikali yake kwa kukijenga na kukiweka jiwe la msingi chuo hicho na kutoa rai kwa vijana wenzake kwenda chuoni hapo kuchangamkia na kupata fursa za ujuzi kupitia mafunzo ya ufundi stadi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages