LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 15, 2024

MCHECHU: WAKATI UMEFIKA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA KUANZA KUWEKEZA NJE YA TANZANIA, RAIS SAMIA KUFUNGUA KIKAOKAZI CHA MA-CEO ARUSHA MWEZI UJAO

Na Bashir Nkoromo, CCM Official Blog, Dar es Salaam
SERIKALI inajipanga kimkakati taasisi na mashirika ya umma yaliyoimarika kiuchumi yaanze kuwekeza nje ya Tanzania kwa lengo la kuimarika zaidi na kuchangia vilivyo uchumi wa Taifa.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu katika mkutanbo wake na Wahariri wa vyombo vya Habari, uliofanyika, jijini Dar es Salaam, leo Julai 15, 2024.

Mchechu amesema, katika hatua za awali, mwezi ujao (Agosti 2024), Serikali itawakutanisha  Wakuu wa Taaasisi, Mashirika ya Umma na Wenyeviti wa Bodi katika Kikao kazi (CEO Forum) kitakachofanyika jijini Aruisha ambacho alisema kitafunguliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema, katika kikao hicho ambacho Wakuu zaidi ya 600 wa Taasisi na Mashirika ya Umma watahudhuria, Rais Dk. Samia pamoja na mambo mengine atatoa maelekezo yake kuwezesha Taasisi na Mashirika ya umma kuweza kuwekeza nje ya Tanzania kwa tija.

Mchechu, amesema Serikali imedhamiria taasisi na mashirika ya umma kuwekeza nje ya nchi kwa sababu hatua hiyo itaongeza wingo wa Taasisi hizo kukua kiuchumi hivyo kukuza pato la taifa.

Alitaja baadhi ya Mashirika yenye sifa ya kuwekeza nje kuwa ni yale ambayo mazingira yake ya kiutendaji yanaruhusu kama Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Reli Tanzania (TRC), huku akitaja sifa za Taasisi kuwa ni uwezo wake kukua kiuchumi kama Benki za NMB, CRDB na TCB.

Mchechu amesema, wakati Serikali ikiwa katika mikakati ya mashirika na taasisi zake kuwekeza nje ya nchi, pia ipo katika kufanya maboresho ya kimsingi kuhakikisha uimara na umadhubuti wa kutosha unakuwepo katika mashirika na taasisi zote.

Amesema katika kuboresha na kuimarisha, hatua mbalimbali  zitafanyika ikiwemo kuhakikisha Wakuu wa Taasisi na Mashirika wanakuwa wenye uwezo unaokidhi na kwamba katika kufanya hivyo wakuu watakaoonekana hawakidhi wataondolewa.

Mchechu alisema, sanjali na hivyo, pia Taasisi na mashirika yatapewa uwanja mpana wa kujisimamia katika uendeshaji, badala ya kusimamiwa na serikali.

“Katika kufanya hivi, baadhi ya mashirika au taasisi kama hazifanyi vizuri zitavunjwa na majukumu yake kuhamishiwa kwingine na taasisi ambazo shughuli zake zinafanana zitaunganishwa au kubadilishiwa majukumu”, amesema Mchechu.

Kuhusu Taasisi na Mashirika ya Umma kuchangia Mfuko wa Serikali, mchechu amesema, sasa jukumu hilo litakuwa ni lazima kwa kila Taasisi na Shirika na fedha za uchagiaji lazima zitokane na mapato ya Taasisi au Kampuni husika.

Akizungumzia utendaji wa Shirika la UDART linalotoa huduma ya mabasi ya mwendo kasi katika jiji la Dar es Salaam na sehemu ya mkoa wa Pwani,  Mchechu amesema Serikali imo kwenye mikakati ya kuhakikisha huduma za shirika hilo zinakuwa bora zaidi.

Amesema katika moja ya hatua ya kuiwezesha UDART, serikali itaipatia mabasi 100 ambayo yatakuwa yanafanya kazi katika njia kuu.

Mchechu amesema, katiika kufanikisha lengo hilo, Ofisi ya Msajili wa Hazina kesho itakutana na watendaji wa benki ya NMB kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji mradi huo.

Amesema mradi wa UDART ni wa uwekezaji mkubwa hivyo unahitaji wawekezaji zaidi ya mmoja ili kuweza kuhudumia njia sita za mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema, kuwa na wawekezaji zaidi ya mmoja kutachochea ufanisi zaidi katika utoaji huduma kutokana na ushindani utakaokuwepo.

Mapema, MKurugenzi wa Idara ya Habari (Melezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba alipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanyakazi zake kwa uwazi hasa kwa kushirikisha sekta mbalimbali.

Amesema, utendaji huo ikiwemo kuvishirikisha vyombo vya habari umewezesha umma kujua kwa undani shughuli za mashirika na taasisi za umma na pia umma huo kujua kwamba taasisi na mashika ni mali yao.

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza katika kikao chake na Wahariri wa Vyombo vya Habari, leo jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza katika kikao chake na Wahariri wa Vyombo vya Habari, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba akizungumza katika mkutano huo.
Baadhi ya Wahariri na Wakuu wa vyombo vya habaru wakiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya Wahariri na Wakuu wa vyombo vya habaru wakiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya Wahariri na Wakuu wa vyombo vya habaru wakiwa kwenye kikao hichoBaadhi ya Wahariri na Wakuu wa vyombo vya habaru wakiwa kwenye kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages