Na HEMEDI MUNGA na SEIF TAKAZA, Iramba
Maandalizi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Iramba mkoani Singida yamekamilika kwa asilimia takribani 100 hadi sasa.
Aidha, Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda ametoa wito kwa wananchi wote wajitokeze Julai 09 kila eneo ambalo tunu hiyo ya Taifa itapita.
Amesema Mwange wa Uhuru katika wilaya hii, utakimbizwa kilometa 68.1 huku ukitembelea, kuona, kuweka mawe ya msingi, kupata taarifa mbalimbali ikiwemo kuizindua miradi saba.
"Niwaombe ndugu zangu wananchi, watumishi wa umma, watumishi wa taasisi mbalimbali na viongozi wa dini kujitokeza kwa wingi kuushangilia Mwenge wa Uhuru mahali popote utakapo pita wilayani kwetu," ameomba DC Mwenda.
Aidha, ameweka wazi miradi itakayopitiwa na kutembelewa na Mwenge wa Uhuru ni mradi elendelevu wa maji kijiji cha Makunda-Uliyang'ombe uliozinduliwa mwaka jana, kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti kijiji cha Kyengege na ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (VETA) eneo la Salala kata ya Old Kiomboi.
Ametaja miradi mingine ni ujenzi wa shule mpya inayoitwa Iramba sekondari iliyopo Kata ya Old kiomboi, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 1.5, ujenzi wa majengo ya huduma ya afya ikiwemo mitambo ya kuzalisha hewa ya oxygen, jengo la Mama na Mtoto na jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya Kiomboi.
"Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali wilaya yetu kuipa fedha nyingi ambazo zimetekeza miradi mbalimbali ya maendeleo," ameshukuru na kuongeza kuwa:
"Miradi yote itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu inagharama ya sh bilioni 5.084."
Mwenge wa Uhuru utapokelewa wilayani Iramba katika kijiji cha Maluga ifikapo mwezi Julai, 09 mwaka huu ukitokea wilaya ya Singida.
Hata hivyo, Mwenge huo, ulipokelewa Julai 05 na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ambae alikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇