LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 24, 2024

DIWANI KIMWANGA: HALI NI SHWARI MAKURUMLA, HAKUNA MTOTO ALIYEKWISHATEKWA

Makurumla, Ubungo, Dar es Salaam

Diwani wa Kata ya Makurumla Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewaasa wazazi na walezi kuwa watulivu dhidi ya taharuki ya utekaji watoto kwenye shule.


Amesema licha y taharuki kuenea hadi ndani ya Kata ya Makurumla hakuna tukio la kutekwa mtoto na kuwataka wazazi  na walezi na kila mwanajamiini kuhakikisha anatoa ulinzi kwa watoto hasa mitaani.


Diwani Kimwanga amesema hayo jana, Julai 23, 2024 alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi na walimu wa shule za Msingi za Mianzini,  Karume na Dk. Omari, kufuatia juzi kuzuka taharuki ya kutekwa watoto kwenye shule hizo, wazazi wakalazimika kuvamia shule kuona usalama wa watoto wao.


"Tangu zilipoibuka taarifa hizi na kuzua taharuki juzi Julai 22, 2024 (Jumatatu), tumefuatilia taarifa kwenye shule zetu, vyombo vya ulinzi na usalama kwa maana ya Jeshi la Polisi hali iko shwari wazazi wenzangu.


Wale waliopata taharuki na kuja shule hawajakosea kwa sababu wamefanya hivyo kwa lengo la kutaka kujua usalama wa watoto. 


Najua mama zetu uchungu mkubwa wanaoupata hasa kuhusu watoto. Wazazi wenzangu naomba tuwe watulivu hali iko shwari kubwa tusisahau wajibu wetu wa malezi na usalama kwa watoto hata wanapokuwa nyumbani na mitaani," alisema Diwani Kimwanga


Sanjari na hilo, Diwani Kimwanga aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa lazima waweke mkazo kwenye suala la lishe kwa watoto kwa kuhakikisha wanachangia fedha ya chakula sh. 500 kika mmoja kama walivyokubaliana kwenye mikutano ya wazazi, jambo ambalo litamsaidia mtoto kupata chakula shuleni badala ya kwenda mitaani wakati wa mapumziko.


Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni naye aliwataka wazazi kuwa na utulivu akisisitiza kuwa hadi kufikia siku ya kijao hicho hakuna taarifa za watoto kutekwa katika shule ndani ya manispaa hiyo.


"Naomba walimu msisahau wajibu wa kuandika mahudhurio ya watoto kila siku wawapo darasani na hata wakati wanapomaliza masomo kwa siku majina yaitwe. Hatua hii ndio njia ya kuendelea kudhibiti usalama wa watoto wetu," alisema Nyoni.


Polisi Kata wa Kata ya Makurumla, Mkaguzi wa Polisi Emmanuel Humba, alithibitisha kwenye kijao hicho kuwa katika Kata hiyo hali ni shwari hakuna tukio la utekaji  watoto huku akiwaomba wazazi kuwa watulivu wanapopata taarifa za taharuki.

Diwani wa Kata ya Makurumla Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, akizungumza na Wazazi, Walezi na Walimu wa shule za Msingi za Mianzini,  Karume na Dk. Omari, katika Kata hiyo, jana.

Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni akizungumza katika mkutano huo.
Polisi Kata wa Kata ya Makurumla, Mkaguzi wa Polisi Emmanuel Humba, akizungumza kwenye mkutano huo.


Wazazi, walezi na Walimu wakiwa kwenye kikao hicho.
Polisi Kata wa Kata ya Makurumla, Mkaguzi wa Polisi Emmanuel Humba (kushoto) akiwa na mwenzake kwenye kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages