Na HEMEDI MUNGA, Iramba
Wananchi mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Iramba Mkoani Singida wameombwa kuwakataa viongozi wa kisiasa ambao wanadaiwa kutoa kauli zinazodaiwa kuwa za kichochezi, kibaguzi na zenye viashiria vya kuvunja amani.
Aidha, wamekumbushwa walikotoka ambapo hakukuwa na maendeleo licha yakuwa na ardhi na mifugo lakini hakukuwa na miundombinu yakupeleka sokoni ukilinganisha na hali iliyopo hivi sasa wanaweza peleka mazao ikiwemo mifugo popote na kwa wakati.
Akizungumza na wananchi hao, katika kiwanja cha stendi ya mabasi mjini Kiomboi wilayani hapa, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Martha Mlata amewaomba wapuuze maneno yoyote yanayosemwa kwa lengo la kutaka kuwapotosha na kuwadanganya watu.
Aidha, amewaomba wananchi hao, kuendelea kumuombea na kumuamini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambae amejitoa kuwaletea maendeleo katika nyanja zote ikiwemo maji, umeme, barabara na elimu.
Hata hivyo, Martha amewakumbusha adha ya usafiri waliokuwa wakiipata zamani ambapo walilazimika kutoka Iramba kwenda kupanda gari Singida mjini kuelekea Dar es Salaam lakini leo hii mabasi yanaanzia safari mjini Kiomboi kwa sababu ya uwepo wa barabara za lami.
Aidha, amesema walilazimika kutumia vibatali wakati wa kujisomea ambavyo viliingiza moshi mapuani hali ambayo hivi sasa haipo kwa sababu Rais Dk. Samia amefikisha umeme katika vijiji vyote, hivyo wanakila sababu ya kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo.
Pia, kuhusu elimu ameeleza watu walikua wanafaulu lakini anayepata bahati ya kuendelea na masomo anawezakuchaguliwa mmoja tu, lakini leo hii shule zimejengwa katika kila kata huku hata watoto wao wakisoma elimu ya awali kwa kutumia zana za kisasa.
Akizungumzia kuhusu Muungano wa Tanzania na Zanzibar, Martha ameweka wazi ni tunu ya Taifa hili, wazee wao waliungana kwa sababu walikua wanataka kuleta maendeleo, hivyo leo wanashuhudia maendeleo lukuki.
Aidha, ameongeza wazee walitaka kulinda amani ya Taifa hili, hivyo watakao waletea maneno kuwa hakuna Muungano wawakatae na wasiwasikilize kwa sababu hawafai.
"Ni lazima tuendelee kutunza amani ya Taifa hili kwa ajili ya vizazi vijavyo, hivyo wakija wakataeni," amesisitiza.
Mbali na hayo, Martha amewaomba viongozi wa dini kukemea wanaomdhihaki kiongozi ambae alichukua nchi katika mazingira magumu lakini aliweza kuwafanya kuwa imara hadi hivi sasa.
"Viongozi wangu wa dini niwaombe muendelee kumuombea Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na kumtaka anayejiita mchungaji anayetamka kuwa Rais amekataliwa na Mungu akatubie kwa kuwa yeye ndio amekataliwa na Mungu kwa kukosa weledi wa kuhutubia," ameomba.
Kwa upande wa Katibu wa Chama hicho mkoa huo, Lucy Shee amesema haikubaliki kwa kiongozi wa chama cha sisasa anaomba kibali cha kuhamasisha na kuimarisha chama chake halafu akiishapanda katika jukwaa anahubiri habari ya kuvunja Muungano.
Amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema atakae anza kusema sisi watanganyika na wao wazanzibari lana itamtafuna ndio maana chama cha kiongozi huyo kinatafunwa na lana kwa sababu ya kutaka kuwarudisha Watanzania kwenye ukabila na ubaguzi wa kidini.
Aidha, amemtaka aliyejiita Mchungaji asitumie kuvuli cha dini kuja kuvuruga amani ya Tanzania na kumchonganisha Rais Dk. Samia na viongozi wa dini kwa sababu wanafahamu namna viongozi hao wanavyomuunga mkono na kushikamana nae.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego ametoa wosia anayemtukana Mama wa mwenzie na wakwake atatukanwa, anayemdharau Mama wa mwenzie na wakwake atadharauliwa na yoyote anayemdharau mwanamke katika dunia hii anahasara.
"Ndugu zangu muogopeni mtu wa namna hiyo alielala tumboni mwa Mama yake miezi tisa halafu leo anasima hadharani kumtukana mwanamke bila woga, hakika huo ni ushetani na Watanzania hatuna tabia hiyo," amesema na kuongeza kuwa:
"Hatutakubali matusi, sio sehemu yake, tunatukanwa matusi wakati tumefanya mambo makubwa."
Amesema Watanzania hatuna mila hiyo kwa sababu siasa ni kupishana kwa maendeleo kuwa wewe utafanya hivi kwa kutumia njia hii na mwingine atafanya hivi kwa kutumia njia ile na sio kutukanana.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amesema hivi karibuni alipita kijana katika wilaya hiyo na kusema Rais hajafanya kitu, jambo ambalo sio kweli, amekosa hoja mtu huyo kwa sababu Rais Dk. Samia ameipendelea Iramba.
Ameongeza zaidi ya sh bilioni 83.7 zililetwa na Rais Dk. Samia katika wilaya hii kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendego akieleza wanavyotembea kifua mbele kwa maendeleo aliyoyafanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika mkoa huo, wakati wa mkutano uliofanyika katika kiwanja cha stendi mjini Kiomboi wilayani Iramba mkoani hapa. (Picha na Hemedi Munga)
Mkuu wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Suleiman Mwenda akieleza sh bilioni 83.7 zilivyowakosesha hoja wapizani Iramba, wakati wa mkutano uliofanyika katika kiwanja cha stendi mjini Kiomboi wilayani Iramba mkoani hapa. (Picha na Hemedi Munga)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇