Na HEMEDI MUNGA, Singida
WAGUSWA wa Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga waliopo mkoani Singida wamekwishalipwa fidia zao na wanafurahia matunda ya mradi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wa mkoa huo, katika semina ya kuwajengea uwezo na kupata taarifa sahihi za mradi huo, iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Ofisa Mahusiano ya Jamii wa mradi huo, Josephath Kanyunyu amesema Waguswa 1296 wameishalipwa fidia zao.
Ameweka wazi zaidi ya asilimia 99 wamelipwa huku Waguswa nane wakiwa bado kwa sababu ya kutosaini mikataba yao kutokana na sababu anuai.
Aidha, amesema makaburi 235 yalihamishwa kwa kuzingatia taratibu za serikali na mila za jamii husika ikiwemo kulipa fidia.
Pia, amesema katika mkoa huo, zilijengwa nyumba 31 ambapo Singida DC 19, wilaya ya Iramba 10 na Mkalama nyumba mbili.
Kwa upande wa Ofisa Mawasiliano wa Mradi huo nchini Tanzania, Abbas Abraham amewaeleza Waandishi hao, mradi huo umefanikiwa kukwepa athari za kimazingira na kijamii.
Amesema wakati wa mradi ardhi ya Waguswa takribani 9,000 kutoka katika mikoa yote ambayo mradi umepita ilichukuliwa na wamekwisha lipwa fidia.
"Zaidi ya asilimia 99 tayari wameishalipwa fidia zao, wapo waliolipwa fedha taslim na wapo waliojengewa nyumba na kukabidhiwa," amesema.
Amebainisha kwa upande wa Tanzania nyumba 339 zilijengwa katika mikoa minane ambapo walengwa waliishakabidhiwa.
"Tumejenga nyumba kwa teknolojia bora inayowezesha kudumu kwa miaka mingi kwa lengo la kuhakikisha Waguswa wananufaika kwa muda mrefu," amesisitiza.
Aidha, ameeleza mbali na hayo, Waguswa walipewa msaada wa chakula kwa kipindi cha mpito kwa lengo la kuhakikisha wanajiweka sawa katika maeneo ambayo wamehamia.
Ameongeza Mradi ulifanya shughuli mbalimbali za kuinua na kuboresha hali za maisha ya Waguswa kwa lengo la kuwaacha wakiwa na hali bora za maisha kuliko walizokuwa nazo zamani.
Akizungumzia kuhusu mashamba, Abraham amesema walioguswa katika mashamba waliyokuwa wanalima walipewa mengine, usaidizi wa kilimo, kufundishwa namna ya kulima kisasa ikiwemo mbolea.
Naye Mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari wa mkoa huo (SINGPRESS), Edina Malekela ametoa wito kwa wasimamizi wa mradi huo kuwashirikisha Waandishi wa Habari kwa sababu Mwandishi anauwezo wa kumfikia mwananchi popote alipo iwe kwa kutumia gazeti, radio, Luninga au mitandao ya kijamii.
Amesema wafanye kazi karibu na wanataaluma hao kwa lengo la kuhakikisha jamii inajua kuwa mradi huo ni salama, unamanufaa na malengo makubwa kwao.
Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda umepita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma hadi Chongoleani jijini Tanga.
Aidha, mkoani Singida umepita katika ardhi yenye urefu wa kilometa 60 wilaya ya Iramba, kilometa 11 wilaya ya Mkalama na kilometa 80 Singida DC.
Mradi huo, unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025 na kuanza kusafirisha mafuta gafi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇