Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog
Moja ya Taasisi zinazosimamiwa na Msajili wa Hazina (OTR), Tanzania Commercial Bank (TCB), imetangaza kutia kibindoni ongezeko la faida ya Sh. Bilioni 10.7 za Kitanzania, baada ya makato ya kodi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ambayo imefikia tamati Machi 31, 2024.
Akiwasilisha utendaji kwenye kikao kazi baina ya TCB na wahariri na waandishi wa habari, kilichoratibiwa na ofisi hiyo ya Msajili wa Hazina, na kufanyika jijini Dar es Salaam, leo Aprili 9, 2024, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Adam Mihayo, amesema Benki inaamini ongezeko hilo ambalo ni asilimia 358 katika mapato yake kipindi cha robo ya kwanza yametokana na ukuaji mkubwa wa mapato katika aina zake zote za biashara na ongezeko kubwa la kitabu cha mizania katika kipindi tajwa kilichopitiwa.
Amesema mapato yaliongezeka kwa asilimia 30 hadi kufikia Sh. Bilioni 56.8 yakiimarishwa na kitabu cha mizania na kasi kubwa ya ukuaji katika mapato yote.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo, ameongeza kuwa, amana za wateja zimeongezeka kwa asilimia 12 kufikia sh. trilioni 1.1 za kitanzania ikiashiria imani kubwa ya wateja wetu kwa benki, wakati huohuo mikopo kwa wateja imepanda kwa asilimia 15.4 kufikia sh. Bilioni 983.6 za kitanzania hadi Machi 31, 2024. "Hii inaonyesha dhamira ya benki katika kuwezesha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu wake", akasema Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
“Ninajivunia kuwatangazia utendaji wetu wa kipekee katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024. Ukuaji mkubwa huu unasukumwa na dhamira yetu ya dhati na kujizatiti kwetu katika ufanisi ili kumridhisha mteja. Sisi ni benki ambayo inachukua muda wake kuwasikiliza wateja wetu na kuweka juhudi katika kuelewa mahitaji yao.
Kwa ongezeko hili la mapato kwa asilimia 30 tumedhihirisha kwa mara nyingine tena ujasiri wetu, na uwezo wetu wa kulikabili soko linalokua kwa kasi. Imani ya wateja wetu kwetu bado ni imara kama inavyothibitishwa na ongezeko la amana ya wateja" , amesema Afisa Mtendaji Mkuu huyo na kuongeza;
"Vile vile, dhamira yetu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi inadhihirika wazi katika ongezeko la mikopo kwa wateja wetu. Tukiendelea na safari hii ya mafanikio, tunajizatiti kuwafikishia watu ubunifu wa kifedha na kuchangia katika ustawi wa watu wetu na Taifa letu kwa ujumla.”
Afisa Mtendaji Mkuu huyo alisema, jumla ya gharama kulingana na kipato katika robo hiyo ya kwanza ni
sh. bilioni 43.2 za kitanzania, sawa na ongezeko la asilimia 6.1, ukilinganisha sh. bilioni 40.7 na robo ya kwanza ya mwaka jana 2023, wakati huohuo jumla ya gharama za uendeshaji ikiwa imepanda kidogo kutoka sh. bilioni 26.5 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi kufikia sh. bilioni 26.8 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2024.
“Tumejizatiti kuendeleza jitihada katika kutekeleza mkakati wetu ambao unazingatia ufanisi wa uendeshaji, na kuendelea kupunguza gharama zetu kwa uwiano wa mapato licha ya kuongezeka kwa kipindi hiki."Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa TBC akasisitiza na kuongeza akisema;
"Benki inahusisha ukuaji huu wa faida na maendeleo endelevu ya biashara ndogondogo na za kati nchini. Hali kadhalika, katika kufikia lengo la benki juu ya wafanyabiashara wadogowadogo na wakati, TCB imetumia njia ya kidigitali katika kufanya ufumbuzi wa kibenki, na hivyo kuwapa wateja wake ufanisi, urahisi na uwezo wa kufanya shughuli za kimiamala.
Mwelekeo huu wa kimkakati unaimarishwa na mkakati wa kidigitali unaoendelea, ambao umeiwezesha benki kuwa karibu zaidi na wateja wake kuliko awali na kuwaruhusu wao kuendelea kujipatia huduma za kibenki katika sehemu zinazowapendeza wao na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya benki na wateja wake".
Kuhusu mtandao wa mawakala wa kibenki wa TCB Benki, Afisa Mtendaji Mkuu huyo akasema umekua kwa
takribani mara nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kutoka idadi ya mawakala 1,584 mwaka 2020 hadi zaidi ya mawakala 6,000 kwa mwaka 2023.
Amesema pia idadi ya mashine za UmojaSwitch za ATM zimeongezeka kutoka 250 mwaka 2020 hadi kufikia mashine 281 kwa mwaka 2023 na kwamba katika kipindi hicho, TCB Bank pia imeanza kutoa kadi za VISA huku akisema pia kwamba Umoja Switch imeingia ubia na Benki ya NMB na katika robo hii ya kwanza ya mwaka 2024, tayari kuna mashine za ATM 750 za NMB ambazo zimeunganishwa na ATM za UmojaSwitch na kufanya jumla ya mashine za ATM za UmojaSwitch kufikia 1,031 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema pia kwamba TCB Benki imeweza kuanzisha bidhaa bora kama, M-Koba, akitamba kwamba ni matumaini ya uongozi wa TCB Bank kwamba wataendelea kutoa bidhaa zinazowalenga wateja ambazo zitaendelea kuvunja rekodi kwa kipindi chote cha mwaka 2024 na kuendelea.
DONDOO
Ukuaji wa Mapato:
Mapato yaliongezeka kwa asilimia 30 hadi sh. Bilioni 56.8. Ukuaji huu uliimarishwa na upanuzi wa kitabu cha mizania na ukuaji thabiti katika nyanja zote za mapato.
Amana za Wateja:
Amana za wateja zilikua kwa asilimia 12 hadi sh. trilioni 1.1. Ongezeko hili linaonyesha imani walioijenga wateja katika benki yetu.
Mikopo ya Wateja:
Mikopo ya Wateja ilipanda kwa asilimia 15.4 hadi sh. Bilioni 983.6 hadi tarehe Machi 31, 2024. Hii inaonyesha
dhamira ya benki katika kusaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wateja wake.
Mikopo Chechefu (NPL):
Mikopo iliyo na ugumu kwa kulipwa ilifikia asilimia 3.97. Asilimia hii inaonyesha sehemu ya mikopo kwingineko
ndani ya benki ambayo iko katika hatari ya kutolipwa au ambayo ina makosa.
Jumla ya Gharama:
Jumla ya gharama katika robo ya kwanza ya mwaka ilifikia sh. bilioni 43.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa na sh. bilioni 40.7 zilizotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2023.
Gharama za Uendeshaji:
Jumla ya gharama za uendeshaji zilipanda kutoka shilingi bilioni 26.5 mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi sh. bilioni 26.8 kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2024.
Kuhusu Tanzania Commercial Bank (TCB):
Ni taasisi ya kifedha ya Tanzania, ambayo imejikita katika kutoka suluhisho la kifedha. Ikiwa na historia pana na uwajibikaji katika kumridhisha mteja, TCB Benki imedhamiria kuwa benki pendwa zaidi na rafiki kwa wateja nchini Tanzania.
Matarajio ya TCB Bank:
Kusonga mbele na mikakati kusudiwa ili kupeleka mbele ukuaji wa Taasisi ya kifedha nchini Tanzania na kuwa taasisi inayoongoza nchini, kwa kutoa huduma ya viwango vya juu kwa wateja wetu na thamani isiyofikika.
Tanzania Commercial Bank imeidhinishwa na inasimamamiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kutoa huduma za kifedha mbalimbali kwa kampuni, biashara ndogondogo na za kati, na kwa watu binafsi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB Adam Mihayo akitoa wasilisho la utekelezaji wa shughuli za benki hiyo mbele ya wahariri na waandishi wa habari, leo.Afisa habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina akiongoza kikao kazi hicho baina ya TCB na Wahariri, leo.
Mkurugenzi wa Masoko na Maendeleo ya Biashara, TCB Deo Kwinyukwa akizungumza kwenya kikao kazi hicho.Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa TCB, Regina Semakafu akizungumza kwenye kikao kazi hicho..Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevil Meena akizungumza katika kikao kazi hicho.
Baadhi ya Wahariri wakiwa kwenye kikao kazi hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya TEF Jane Mihanji akiwa kwenye kikao kazi hicho.
Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri (kushoto) akimshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB Adam Mihayo mwishoni mwa kikao kazi hicho.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇