*KOCHA SIMBA AOMBA RADHI,
*YANGA
*DK SAMIA AWATUMIA SALAAM
Na Ibrahim Bakari, CCM Blog
Wakati kocha wa Simba Abdelhaik akiomba radhi mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Simba kwa timu kufanya vibaya, Yanga wamesema watalidai bao lao Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Benchikha amesema Simba imepoteza mchezo, lakini kwa sehemu kubwa wamepambana dhidi ya Al Ahly na hata hivyo, bahati haikuwa yao.
Simba imetolewa kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya kufungwa bao 1-0 mchezo wa kwanza lakini marudiano ikafungwa mabao 2-0.
Benchikha amesema kwa sasa wanaelekeza nguvu mechi za Ligi Kuu na ataendelea kukiimarisha kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mashindano hayo msimu ujao.
Wakati hayo yakijiri kwa Simba, mahasimu wao, Yanga kupitia Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said amesema tayari wametuma malalamiko yao CAF kulalamikia bao lao lililokataliwa.
Yanga ilipata bao katika dakika ya 59 lililowekwa kambani na Aziz Ki lakini Mwamuzi Dahane Beida kutoka Mauritania alilikataa bao hilo.
Mwamuzi huyo ameifanya uamuzi wa moja kwa moja kulikataa bao badala ya kutumia VAR kujiridhisha baada ya kuonekana kuwepo kwa utata.
Hersi amesema kuwa wamekamilisha utaratibu wote kwa mujibu wa Kanuni za CAF, kukata rufani pamoja na kuwasilisha malalamiko.
Yanga imetolewa kwa jumla ya mikwaju 3-2 ya penalti baada ya timu hizo kumaliza dakika 180 zikiwa suluhu.
Wakati Yanga ikikata rufani, Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amesema pamoja na Yanga kukata rufani, CAF haitabadilisha matokeo ya mchezo huo.
Akizungumzia hatua ya Yanga kukata rufani, Rage amesema itakachofanya CAF ni kumwadhibu mwamuzi, lakini si kubatilisha matokeo ya mchezo huo.
Katika hatua nyingine, timu za Esperance ya Tunisia na TP Mazembe ya DR Congo zinaungana na Al Ahly na Mamelodi kuingia nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa ya klabu Afrika.
TP Mazembe imeitupa nje ya michuano hiyo, Petro Atletico ya Angola wakati Esperance iliitoa ASEC Mimosa ya Ivory Coast.
Wakati huo huo, Rais Dk Samia Suluhu amezitumia salaam Simba na Yanga akizitaka kuongeza bidii kwenye mashindano yajao.
Amesema kuwa Serikali yake itaendelea kuwaunga mkono kwenye ushiriki wa mashindsano hayo ngazi ya klabu mwakani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇