Na Hemedi Munga, Iramba
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amewaomba wananchi kuendelea kumshukuru na kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu anaendelea kufanya makubwa yanayoboresha ustawi na kujali afya zao.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Urughu, wilayani Iramba mkoani Singida. Dk. Nchemba amesema rais samia anagusa maisha ya mtu mmoja mmoja nchini.
Ameweka wazi kuwa fedha zinazokuja Iramba na maeneo yote ya nchi zinakwenda ikiwemo kujenga vituo vya afya katika kila tarafa na maeneo muhimu nchini.
"Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu, anafanya mambo makubwa, fedha alizozitoa haziishii kwenye makaratasi ni vituo vya afya vinavyoonekana kwa macho kote nchini, mtu anaejali afya yako amekutakia mema sana kwa sababu bila ya afya huwezi kufanya kazi," amebainisha. .
Aidha, ameeleza kuwa mtu anaejali afya yako anakupa mtaji wa kufanya kazi kwa sababu mtu anaweza kuwa na mipango mizuri ya kazi lakini asipokua na afya njema hawezi kuitekeleza mipango hiyo.
Aliongeza kuwa hatua hiyo, ndio tafsiri halisi ya Rais Dk Samia kuwapenda watanzania maana vituo hivi mnavyoviona hapa vipo nchi nzima.
"Ndugu zangu ninawathibitisha kuwa nchi nzima katika kila makao makuu ya tarafa na eneo la kimkakati lisilokua tarafa kuna kituo cha afya chenye hadhi ya hospitali ya wilaya," amesisitiza na kuongeza kuwa.
"Mama ametafasiri kwa vitendo kauli ya kuwapenda Watanzania na anashughulikia tatizo la ugumu wa maisha kwa kupeleka miradi mikubwa ya umwagiliaji hata ngazi ya kijiji ambayo inatoa majawabu."
Amesema anaorodha ya matatizo na kutoa majawabu kivitendo kwa sababu nchi nzima kuna miradi ya umwagiliaji na miradi ya kufungua barabara ambapo itabadilisha maisha ya watanzania kutoka kwenye ugumu.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amedokeza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alihakikisha usalama wa chakula na kilimo kwa kuagiza yachaguliwe maeneo kwa lengo la kupanua na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
Amesema hatua hiyo, itawafanya wananchi waweze kulima wakati wote wa kiangazi na masika kwa sababu watakua wanauwezo wa kuhifadhi maji.
"Tunao mradi wa Masimba katika sehemu ya Bonde la Wembere ambapo tumeishaletewa zaidi ya sh bilioni 3 na kutenga hekari 36,000 ambazo zitaendelezwa kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji," amesema DC Mwenda.
Aidha, amethibitisha kuwa tayari wataalam, maofisa wa umwagiliaji watatu wameishafika kujitambulisha ofisini kwake ambao wanashirikiana na wenyeji na kazi tayari imeanza.
Mkuu wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Suleiman Mwenda akithibitisha kupokea takribani sh bilioni 3 katika mradi wa umwagiliaji kijiji cha Masimba kata ya Urughu, leo wakati akiongea na wananchi hao.(Picha zote na Hemedi Munga).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇