Mpanda, Katavi
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emanuel Nchimbi, amesema ndani ya chama bado kuna changamoto ya watu wachache lakini wenye madhara makubwa, wenye tabia ya kupenda kukataa matokeo ya uchaguzi.
Balozi Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo jana, Aprili 13, 2024, akizungumza na viongozi wa CCM Mkoa wa Katavi, na hotuba yake kurushwa mubashara kupitia Channel ten na mitandao mingine ya kijamii.
“Katika chama chetu tunayo changamoto moja, wanaoshinda mioyoni mwao wanakataa matokeo na walioshindwa mioyoni mwao wanakataa matokeo.
Si wengi lakini wana madhara makubwa, mtu anachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi lakini akishamaliza kuchaguliwa anaanza kutafuta nani wa hawakumuunga mkono aanze kupambana nao, katika akili yake amejitengeneza yeye Mungu mtu na kila mtu amchague yeye,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Balozi Dk. Nchimbi ametahadharisha kwamba tabia hiyo kwa baadhi ya wana CCM kukataa matokeo inaleta taswira mbaya kwa vyama vingine vya siasa.
“Tukiwa chama kinachotawala kinachopaswa kutoa muelekeo na dira ya nchi, tunayofanya sisi ndani ya CCM ndiyo yanaakisiwa na vyama vingine. Mkiona vyama vingine vidogo vinaanza kukataa matokeo vinatuiga sisi tunavyokataa matokeo yetu wenyewe. Ndani mtu unapigwa mchana kweupe halafu unakataa matokeo,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Katibu huyo wa CCM amewataka wanachama wa chama wa CCM kujenga desturi ya kuheshimu matokeo ya chaguzi.
“Tujue chama cha siasa madhubuti kinaongozwa na misingi ya demokrasia na demokrasia ya kweli kushiriki chaguzi huru na kukubali matokeo bila kusita. Mimi hapa nimegombea mara 28 na nimeshindwa mara nne na nimeshindwa vizuri sio kushindwa kidogo waswahili wanasema nimepigwa 'flat' mara nne lakini nimegombea nikijua kwamba huu ni uchaguzi kuna kushinda na kushindwa,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Katibu Mkuu Balozi Nchini amefika Katavi akiwa katika ziara ya kikazi, kukagua na kuimarisha uhai wa Chama, akiambatana na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Amos Makalla na Katibu wa NEC Oganaizesheni Issa Haji Gavu, ziara ambayo atafika pia katika Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇