Machi 19, 2021, akiwa amevalia kilemba chekundu na gauni jeusi, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan anashika kitabu kitakatifu cha Quran, akiwa ametulia na kuapa.
Dk. Samia aliapa Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, na kuahidi kuitumikia Tanzania akiwa Rais huku akimuomba Mungu amsaidie.
Hiyo ilifanyika ikiwa ni siku mbili tu baada ya kifo cha mtangulizi wake, hayati John Pombe Magufuli aliyefariki kwa kile kilichoelezwa, ugonjwa wa moyo.
Siku chache baada ya kuapa, wapo walioanza kuwa na wasiwasi na Rais Samia kwa kuwa ni mara ya kwanza Tanzania kuongozwa na Rais mwanamke.
Ni pale alipowakata maini kwa kuwaambia katika moja ya hotuba yake kuwa kwa wale wenye mashaka aliwaambia: “aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke. Kauli hiyo iliwanyamazisha waliokuwa wakibeza na akaonyesha kweli anaweza.
Ifikapo Machi 19, 2024, Rais Dk Samia anatimiza miaka mitatu madarakani na katika kipindi hicho, ameonesha kuwa ni mwanamama wa namna gani.
Ameonyesha ujasiri, uthubutu, umakini lakini kati ya yote utekelezaji wa majukumu ikiwemo mipango mkakati na haki. Rais Samia ni muumini wa haki.
Baada ya kuapa, Dk Samia, hakutaka kubaki ofisini, alisoma sura za Watanzania nakusema anataka kufungua uchumi na hawezi kuongoza watu wenye masononeko mifukoni.
Ukiacha hayo katika siku 1,095 Rais amejielekeza kwenye mambo mbalimbali ya msingi kama ifuatavyo:
HUDUMA ZA KIJAMII
Kikubwa anachokipigania hadi leo ni kumtua ndoo mama kichwani. Hiyo peke yake ni utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Rais hakuona taabu na katika mwaka wa fedha 2023/2024 aliridhia mpango wa ukamilishwaji wa miradi 1,546 ya maji katika mikoa 25 ya Tanzania.
Hadi kufikia Desemba 2023 jumla ya miradi 374 iliyogharimu Sh 128,177,655,882 ilikuwa imekamilika na Serikali inaendelea na ukamilishaji wa miradi mingine 1,172 kupitia Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira ‘RUWASA’.
Eneo la afya ni kama amewabeba Watanzania, kwani Rais amepeleka Sh 6.7 trilioni kwajili ya upatikanaji dawa, vifaatiba na vitendanishi, kuongeza wahudumu wa afya na kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa afya kupitia Samia Scholarship.
Katika elimu, kila mmoja ametakiwa kupeleka mtoto shule kwa kuwa elimu ni bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, huku serikali ikibeba dhamana kwa kutoa ruzuku kwenye shule.
NISHATI YA UMEME
Ukamilishwaji wa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu NyerereJNHPP lililoko Rufiji mkoa wa Pwani, ni kielelezo tosha.
Bwawa hilo ambalo Dk Samia anapigana kumalizika kwake, katika awamu yake ndani ya siku 1,095, tayari mashine mbili zimewashwa kwa majaribio huku umeme wa megawati 235 ukiingizwa gridi ya taifa.
Serikali imeelekeza fedha zaidi JNHPP ambazo awali ilielezwa hadi kukamilika mradi utagharimu Sh 6.558 trilioni na kuzalisha megawati 2,115 utakaokuwa na ziada ya kuuza nje.
Rais Samia amekuwa akihangaika duniani kwa ajili ya kusaka fedha kukamilisha mradi wenyewe kwa ajili ya Watanzania ambapo utakapokamilika, utashusha gharama za umeme.
Pia uanzishwaji wa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme katika maeneo mengi nchini ikiwemo kuhakikisha kila kijiji Tanzania kinapata nishati hiyo.
Itakumbukwa, Desemba 19, 2022 wakati wa kusaini mikataba ya Peri Urban wenye thamani ya Shs 76.9 bilioni kwa ajili kupeleka umeme mikoa ya pembezoni, Rais Samia alisema vijiji vyote Tanzania vitafikiwa na umeme kabla ya mwaka 2025.
BARABARA NA RELI
Rais Samia hakubaki nyuma kwenye ujenzi na uchukuzi kwa rukhsa yake kuidhinishwa kwa Sh 3.554 trilioni.
Fedha hizo ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, vivuko, meli, majengo ya serikali, ununuzi wa ndege na reli hasa ya SGR ambayo ameagiza hadi kufikia Julai mwaka huu iwe imekamilika.
Hayo na mengine, yako ndani ya utaratibu wa utekelezaji wa ilani katika miaka mitatu tu ya Dk. Samia.
KILIMO
Kati ya maeneo ambayo Rais Samia ndani ya siku zake 1,095 ametoa fedha nyingi ni katika kilimo.
Mpango wa Rais ni kuona kila sekta inayoguswa na kilimo, inakuwa na wepesi kwa ajili ya wananchi na serikali kuzalisha chakula na miundombinu yake.
Utoaji wa ruzuku za mbegu na mbolea kwa wakulima, uzalishaji wa miche bora, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula, mafunzo kwa maafisa ugani na uwezeshwaji wao, dawa za kilimo ni kati ya vitu ambavyo Rais Samia anavisimamia.
Kwa mara ya kwanza, bajeti ya kilimo iliongeeka hadi kufikia Sh 19,555,624,000 kwa mwaka 2023/24 ambazo ziliombwa na Wizara husika kwa ajili ya utekeleaji wa miradi mbalimbali ya kilimo na matumizi mengine.
UCHUMI
Katika moja ya hotuba zake, aliwahi kuwaambia wananchi, kuwa wapo wanaotaka masuala ya kisiasa kwa sasa ikiwemo Katiba mpya, hayo yatakuja, lakini kwa sasa aachwe afanye kazi ya kuufungua uchumi.
Mambo mengi ya kiuchumi yalijifunga kwa hiyo kuna kazi ya kuyafungua.
Hata hivyo amesema anahitaji rasilimali fedha katika kutoa huduma za kijamii na zaidi ni kuangalia vipaumbele vya wananchi.
Katika kuinua uchumi, njia pekee nikutengeneza mazingira wezeshi kupitia kituo cha uwekezaji ikiwemo kufungua dirisha moja (one stop), kushawishi wawekezaji wengi kuja kuwekeza na mambo mengine, hiyo pekee itasaidia Watanzania kupata ajira na taifa kuingiza mapato.
Uwezeshwaji kiuchumi wa makundi ya kijamii, wanawake, vijana, walemavu pamoja na kuvipa sapoti vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali.
Uimarishaji wa lango kuu la biashara, Bandari ya Dar es Salaam pamoja na Tanga, Mtwara, Bandari za Kilwa na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Pia Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dk Samia imeelekea nguvu katika kuimarisha bandari zote kwenye maziwa; Victoria, Nyasa, Tanganyika pamoja na ujenzi na ufufuaji wa meli kwa ajili ya kufanya huduma za kiuchumi na kijamii.
Rais Samia amediriki kucheza filamu ya The Tanzania Royal Tour, lengo ni kuitangaza Tanzania na zaidi kuingiza fedha ambapo kwa mara ya kwanza imevuta watalii wengi kuliko kipindi kingine chochote miaka ya nyuma.
Takwimu za hivi karibuni za Baraza la Utalii Duniani inaonesha asilimia 90.7 ya wageni waliingia Tanzania kutembelea vivutio na fukwe za Zanzibar.Aidha mpango mwingine nikuimarisha uchumi wa buluu kwa kuinadi Zanzibar kimataifa.
Hayo na mengine yanabebwa na uimarishwaji wa diplomasia ya uchumi ambayo ndiyo msingi madhubuti wa ushirikiano wa Tanzania na mataifa ya nje hasa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.
MICHEZO
Tanzania kuweka historia chini ya Rais Samia, kuingiza timu mbili robo fainali Ligi ya Mabingwa, ni kielelezo tosha cha msukumo wa ‘Bao la Mama’.
Rais Samia amekuwa akitoa fedha kwa kila goli linapofungwa kwa Simba na Yanga tangu hatua ya makundi ikiwa ni hamasa na hakika amefanikisha.
Simba imepangwa kucheza na Al Ahly ya Misri kati ya Machi 29 na 31 sawa na Yanga itakayocheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika robo fainali.
Katika kipindi cha Rais Samia, motisha yake kwa Taifa Stars imeiwezesha timu hiyo kucheza fainali za AFCON kwa mara ya tatu, zilizofanyika Ivory Coast.
Aidha Tanzania itakuwa taifa mwenyeji wa Fainali za CHAN kwa wachezaji wa ndani Septemba mwaka huu lakini pia mwenyeji wa AFCON ikiandaa kwa pamoja na Kenya na Uganda mwaka 2027.
Kwa upande mwingine, timu za vijana za umri mbalimbali zimeibuka kwa kufanya vizuri katika mashindano yao, timu za walemavu, pamoja na timu za wanawake ikiwemo Twiga Stars.
Kwa mara ya kwanza, Rais Samia ameanzisha harambee maalumu kwa ajili ya timu za Tanzania kwa mashindano ya kimataifa, na kupatikana Sh bilioni 4 ambazo tayari sehemu yake imepeleka wachezaji wa Tanzania katika Michezo ya Afrika huko Ghana.
Pia zitatumika kamasehemu ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika kwenye jiji la Paris, Ufaransa kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11.
SIASA
Kati ya awamu ambazo vyama vya siasa hasa vya upinzani vinapumua, ni awamu hii.
Rais Samia ametumia nafasi yake kuwaruhusu wapinzani hasa CHADEMA kufanya mikutano ya kisiasana maandamano pamoja na vyama vingine huku akisisitiza siasa za kistaarabu.
Hali hiyo pekee imesaidia kushusha joto la wapinzani kuona wanabanwa.
Njia hiyo itawafanya wapinzani kufilisika kwa kila wanachotaka kufanya kwa kuwa rukhsa imetolewa alimradi hawavunji sharia.
Hayo ni kwa uchache, yako mengi ikiwemo ushirikiano wa kimataifa, ushirikiano na mashirika na taasisi wahisani na hata wafadhili.
Dk. Samia Suluhu Hassan akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇