Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM.
Mfuko wa SELF (Self Microfinance Fund) umesema hadi kufikia Disemba 31, 2023, ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 324 (Sh. 324,506,402,014) ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10.
Umesema, mikopo hiyo iliwafikia wanufaika wapatao 314,055; kati yao wanawake 166,449 sawa na asilimia 53 na wanaume 147,606 sawa na asimia 47, na wananufaika hao ni kutoka mikoa 30 ya Tanzania Bara na Visiwani.
Takwimu hizo zimetajwa katika kikao kazi cha Mfuko huo kunadi kwa umma utendaji wake, kupitia kikao kazi baina yake na Wahariri na Waandishi wa habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, na kufanyika leo Machi 11, 2024, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Mfuko huo Afisa Mtendaji Mkuu Mudith Cheyo na Mkurugenzi wa Biashara na Masoko Peter Mataba, walisema, katika kipindi chote tangu taasisi hiyo ilipoundwa, imekuwa ikifanya kazi ambayo imekidhi lengo la kuanzishwa kwake.
Viongozi hao wamesema, hadi sasa Mfuko huo unajiendesha bila kuhitaji ruzuku ya serikali na tena unajiendesha kwa kupata faida na kutoa gawiwo kwa serikali kila mwaka na kuongeza kuwa hadi sasa Mfuko wa SELF Microfinance Fund, umekopesha taasisi ndogo za fedha zaidi ya 200 nchi nzima, sanjari na kuzijengea uwezo taasisi hizo.
Halikadhalika Mfuko umesaidia kutengeneza ajira kwa wakopaji kwa wao wenyewe na wale wanaoajiriwa, kiasi cha ajira 37,024 kimetengenezwa kwa mwaka 2023 na kutoa elimu ya fedha kwa mwaka 2023 ambapo Mfuko uliweza kutoa elimu ya fedha wa wakopaji 1,519
Kuhusu aina za Mikopo inayotolewa na Mfuko wa SELF, Mataba alisema ni pamoja na Mikopo kwa taasisi ndogo za fedha-MFIs/SACCOS akifafanua kuwa Mikopo hiyo inalenga wanufaika wanaofanya biashara au kilimo, mikopo ambayo riba ni kati ya asilimia 16 hadi18 kwa mwaka, mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika ambayo walengwa ni wajasiriamali wadogo na wakati-MSMEs, wakulima wadogo/wafugaji, kwa ajili ya kuboresha makazi, vikundi, kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na mikopo kwa ajili ya watumishi wa umma na riba ya mikopo hiyo ni kati ya asilimia 15 na 22.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo wa SELF (SELF Microfinance Fund) Cheyo, amesema SELF MF ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha ambayo ni zao la Mradi wa Serikali ambao ulijulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility-SELF ulioanzishwa mwaka 1999, Dira ikiwa ni kutoa huduma ndogo za fedha inayoongoza katika kubadili maisha ya watu.
"Mradi wa SELF ulikuwa ni miongoni mwa programu za Serikali zinazotekeleza jukumu la kupunguza umaskini kwa niaba ya Serikali ambayo ilifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Mradi ulilenga katika kuongeza mchango wa biashara ndogo za kati, katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuimarisha tasnia ya mikopo midogo midogo nchini Tanzania kupitia; Mfuko wa mkopo wa jumla kwa Taasisi Ndogo za Fedha zinazostahiki (MFIs), kuimarisha uwezo wa kushirikiana MFIs kupitia mafunzo na usaidizi wa kitaasisi na kukuza na kuhamasisha uundwaji wa MFIs mpya za msingi", alisema, Akizungumzia historia ya Mfuko huo, Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF (Self Microfinance Fund) Mudith Cheyo akiwasilisha utendaji wa Mfuko huo, katika kikao kazi baina ya Mfuko na Wahariri na Waandishi wa Habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa hazina na kufanyika jijini Dar es Salaam, leo Machi 11 2024.






















No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇