Kisesa, Mwanza
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salaam za pole kwa familia ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima na mume wake Wakili Methusela Gwajima kufuatia msiba wa mama mzazi wa Wakili Gwajima uliotokea Machi 27, 2024.
Salaam zilitolewa na mwakilishi Binafsi wa Rais Bi. Sabah Salum, aliyeungana na waombolezaji kwenye kutoa heshima za mwisho nyumbani kwa Wakili Gwajima, Salasala jijini Dar es Salaam, Machi 29, 2024, na baadae salaam hizo kufikishwa kwenye ibada kuu ya maziko nyumbani kwa marehemu Kisesa, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza jana, Machi 30, 2024.
Akitoa neno la shukurani katika ibada hiyo, Waziri Dk. Gwajima alimshukuru Rais Samia, kwa neno la faraja na kuwashika mkono kwenye mahitaji yote ya hafla ya mwisho ya kumuaga mpendwa mama yao.
“Ndugu zangu salaam nyingi za upendo na faraja kutoka kwa Rais Dk. Samia, ambaye jana alimtuma mwakilishi wake binafsi Bi. Sabah Salum, aungane nasi kwenye ibada ya kumuaga mama kule Dar es Salaam na ambaye alitukabidhi rambirambi za Mhe. Rais ambayo ndiyo imewezesha huduma zote za mahitaji ya chakula kipindi chote cha msiba huu hivyo, hatuna budi kutambua upendo huu na heshima hii kubwa” alisema Waziri Dk. Gwajima.
Akitoa shukrani za familia kwa ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki ibada hiyo, Wakili Gwajima pia amemshukuru Rais Samia, kwa kuwapa faraja na heshima kubwa familia yake kwa msiba huo mzito.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, vyama vya Siasa, Makundi ya wadau wameshiriki ibada hiyo ya maziko iliyofanyika Kisesa, wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Machi 30, 2024.
Rais Dk. Samia
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇