LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 20, 2024

BALOZI DK. NCHIMBI: WATANZANIA TUNAJIVUNIA UWEZO MKUBWA WA RAIS DK. SAMIA ANAOONESHA NDANI YA MIAKA MITATU

Victoaria Falls, Zimbabwe

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel  Nchimbi, amesema Watanzania wanajivunia uwezo mkubwa wa kiuongozi, anaouonesha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake.


Balozi Dk. Nchimbi amesema uwezo wa Rais Dk. Samia, umejidhihirisha kwa namna anavyoiongoza nchi, kwa ajili ya maendeleo ya watu, ustawi wa jamii na kuimarisha utaifa nchini.


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Makatibu Wakuu wa vyama rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, unaoendelea katika Mji wa Victoria Falls,  Zimbabwe, jana Machi 19, 2024, Balozi Dk. Nchimbi, amesema pia CCM inajivunia uongozi wa Rais Dk. Samia, kwa jinsi anavyoendelea kuiongoza Serikali katika kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, akisisitiza kuwa CCM na wanaCCM wanamuunga mkono bega kwa bega. 


“Kabla sijaanza kuwasilisha hapa, kwa ruhusa yako Mwenyekiti wa kikao hiki, imekuwa kama bahati nzuri zilizogongana leo. Naomba niwataarifu Wajumbe wa Mkutano huu kwamba leo ni maadhimisho ya mwaka wa tatu tangu Mhe. Samia aliposhika madaraka ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania miaka mitatu iliyopita.


Kwa kweli ninajivunia sana Rais Samia, si kwa sababu tu mimi ni mpigania haki za wanawake, bali kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa uongozi mzuri anavyoendelea kuiongoza nchi yetu ya Tanzania. 


Kutokana na hilo, CCM inajivunia sana uongozi wake, na Watanzania kwa ujumla wetu tunajivunia sana kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwezo wake mkubwa ambao ameuonesha ndani ya hii miaka mitatu,” amesema Katibu Mkuu Balozi Dk. Nchimbi.


Dk. Nchimbi pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wajumbe kuwa kutokana na kuwa mwanamajumui wa kweli wa Afrika, Rais Dk. Samia ana dhamira ya dhati ya kuimarisha na kuboresha uhusiano wa nchi na vyama rafiki katika ukombozi kusini mwa Afrika na kwamba anafuatilia mkutano huo kwa ukaribu.


Aliwaomba wajumbe kuungana nae kumtakia kila la heri Rais Dk. Samia na kumuunga mkono, ombi ambalo lilipokelewa na kukubaliwa na wajumbe.

Balozi Dk. Nchimbi akizungumza katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages