LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 21, 2024

KINANA AFUNGUKA MASWALI YA WAANDISHI WA HABARI

Na Jacqueline Liana, Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ni chama kinachotoa uongozi wa nchi tangu kilipozaliwa Februari 5, 1977, kikibeba wajibu wa kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo.


CCM kimepata mafanikio ya kupigiwa mfano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kudhihirisha umadhubuti kwa kuwa chama tegemeo la Watanzania kwa miaka mingi ijayo.

 

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, hivi karibuni alijibu maswali ya waandishi wa habari wa gazeti la ‘Uhuru ya Kijani, waliotaka kujua mambo anuai kuhusu na chama hicho.

 

SWALI: Mwaka huu wa 2024, Chama Cha Mapinduzi kimetimiza miaka 47 tangu kilipozaliwa, je, kwa umri huo, ni kwa vipi  kimetimiza azma ya kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi?

 

JIBU: Ni kweli, malengo na madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Kutokana na mazingira, nyakati na mahitaji; yamefanya makundi mengine yawepo. Mfano, makundi ya wajasiriamali wa chini na wakati,

makundi ya wafanyabiashara wanaofanya biashara zao halali.

 

Hili nalo ni jambo muhimu, kulifahamu, makundi ambayo yapo katika sekta binafsi, kwa sababu sekta binafsi ina nafasi yake kubwa. Lazima mkumbuke kwamba Chama Cha Mapinduzi kilipoundwa mwaka 1977 kilitamka wazi kuwa ni chama cha wakulima na wafugaji, lakini baadaye mwaka 1986 na 1987 yalifanyika mageuzi kiuchumi katika taifa letu ambayo Halmashauri Kuu ya Taifa yaliyajadili na kupitisha mageuzi hayo, na kutoa nafasi kwa sekta binafsi kuendesha uchumi wa taifa letu. Sekta binafsi maana yake ni nini, maana ni wakulima, wajasiriamali wadogo, wajasiriamali wa kati kama vile tunatambua nafasi ya watu wanaofanya shughuli ndogondogo za kujitegemea kama bodaboda, mama ntilie, wanaouza bidhaa mjini na mitaani na kadhalika.

 

Ni kweli Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikipanua fursa za shughuli mbalimbali za uchumi kwa Watanzania, kwa kuzingatia madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi na vile kuzingatia mabadiliko, mageuzi na mahitaji ya wakati, ndiyo maana unaona kwa mfano, tumeweza kuthamini mchango wa makundi mbalimbali katika ujenzi wa nchi.

 

Na ndiyo maana kuna sera za mikopo za wajasiriamali za asilimia 10, katika halmashauri na majiji yetu kusaidia kina mama, wazee na watu wenye ulemavu; makundi ambayo huko nyuma mwaka 1977 wakati Chama kinazaliwa yalikuwa hayapo.

 

Hivyo ni lazima tukiri wakati tunaadhimisha miaka hii 47,  CCM inalinda na kuzingatia misingi yake ya kuthamini uhuru wa mwanadamu na kulinda demokrasia, mazingira na mahitaji ya wakati kila yanapojitokeza.

 

SWALI: Ni upi umadhubuti wa CCM katika demokrasia ya vyama vingi nchini?

 

JIBU: CCM imeendelea kuzingatia mambo makuu manne; la kwanza kujali misingi ya uanzishwaji wake, kutekeleza mahitaji ya Watanzania, kuheshimu utu wa kila mtu, nne ni kuendelea kukuza demokrasia.

 

Nyinyi ni mashahidi; tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza, demokrasia imekuwa ikikua nchini, nafasi ya vyama vya siasa, jamii kwa makundi mbalimbali, yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.

 

Kila unapojitokeza uchaguzi, nafasi za uchaguzi, vyama vimekuwa vikishiriki uchaguzi na kushinda na CCM imekuwa ikikubali wakati wote, kumekuwa na vyama tofauti tofauti katika bunge la Tanzania, vyama vinavyoshindana na CCM vimekuwa vikiongezeka na wakati mwingine kupungua,  viti vya ubunge kwa CCM navyo vimekuwa vikiongezeka na wakati mwingine vikipungua.           

 

Kwa maana hiyo, umadhubuti wetu utaamuliwa zaidi namna tunavyozingatia misingi, maadili na kanuni za chama chetu, kuthamini uhusiano wa chama na Watanzania na kuheshimu matakwa ya Watanzania na mahitaji yao na jambo kubwa linalobaki ni spidi gani inayotumika kuwaletea maendeleo na kujibu hoja zao mara kwa mara.

 

Mimi nadhani, ushindi wa Chama Cha Mapinduzi, ushindi wa kuendelea kupewa ridhaa na Watanzania ni ushahidi dhahiri kuwa tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini, Watanzania wamekuwa na imani na ilani, ahadi, oongozi na usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi kwa utendaji wa serikali ya CCM kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatimia. Iwapo itaendelea  kwa ‘spidi’ kujibu hoja zao kwa vitendo, CCM itabaki madhubuti, itaendelea kuaminiwa na kupewa ridhaa uongozi na Watanzania.

 

SWALI:  Mwaka huu wa 2024 ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa, ni zipi kete za CCM za kuipatia ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo?

 

JIBU: CCM ina historia kila baada ya miaka mitano inaandaa ilani ya uchaguzi na katika uchaguzi wa serikali za mitaa huwa inaandaa tamko, ni dhahiri kwa mwaka huu 2024, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imekuwa na mafanikio makubwa katika kila sekta, huduma za jamii zimepanuka, zimeongezeka. Nina imani mafanikio hayo ndiyo yanaipa mambo matatu makubwa, ambayo ni kete za kuipa ushindi CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.

 

CCM imejipanga kupata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ikijivunia; utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, kuteua wagombea bora na uadilifu wa viongozi. Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025, umefanyika kwa kiwango kikubwa baada ya serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati. Rais Samia Suluhu Hasssan, ameongoza serikali katika kuboresha sekta mbalimbali.


Mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), alipopokea madaraka alichukua mradi ukiwa asilimia 30 lakini sasa ni asilimia 90, Reli ya Kisasa (SGR), barabara na uboreshaji mkubwa katika sekta ya maji, elimu, afya na umeme, umefanyika. Kukamilika bwawa la Nyerere kutachochea ukuaji wa uchumi kwa sababu Tanzania itakuwa na umeme wa kutosha ambao utaleta ustawi kwa wananchi kwa kupata fursa ya kufanya shughuli zitakazowaingizia kipato.


Tangu Rais Samia ameingia madarakani, kumekuwa na maendeleo makubwa katika ujenzi wa barabara, napongeza utendaji wa TARURA kwa kufanya kazi nzuri katika maeneo ya vijijini. Upo ushahidi wa kutosha wa kitakwimu wa mafanikio makubwa katika kila sekta. Maji yamefika katika maeneo mengi, umeme umefika sehemu kubwa, sekta ya afya imefanya vizuri tumeona ujenzi mkubwa wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, vifaa na wameajiriwa watumishi wengi wa huduma za afya.


Sekta ya elimu; imepata mafanikio ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 20,000, ajira kwa walimu wengi, vifaa vya kusaidia mafunzo na ujenzi wa kampasi 14 katika mikoa 14 nchini unaendelea. Umeme umefikishwa kwa asilimia zaidi ya 80 katika maeneo ya mijini na vijijini, na serikali hivi sasa imeanza kujipanga kufikisha katika vitongoji. Kuongezeka kwa mapato ya serikali kumewezesha serikali kutekeleza yote hayo. Lengo ni kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa kikamilifu.


Nina uhakika na sina shaka hata kidogo wananchi wataendelea kuichagua CCM, kwa sababu tuna mkataba kati ya Watanzania na CCM, na mtekelezaji wa mkataba ni serikali.


Ninyi ni mashahidi kutokana na taarifa mbalimbali za maandishi za hotuba zinazotolewa na watendaji, rais, makamu wa rais,   waziri mkuu na mawaziri zimekuwa zikieleza utekelezaji wa ilani unavyofanyika kwa kiwango cha kuridhisha sana. Bila kuelezea kila jambo, lazima tukiri utekelezaji wa ilani umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.


CCM inazingatia  uadilifu kwa viongozi kusimamia vyema wanachokisema na wanachokitenda kwa wananchi, na kete ya tatu ni kuteua wagombea wanaokubalika katika jamii. Tunachosisitia ni wagombea wasiteuliwe kuwania nafasi za uongozi kwa misingi ya rushwa, upendeleo au urafiki, watakaopata fursa ya kufanya uteuzi katika uchaguzi huo, wachague wagombea wenye heshima katika jamii.


Lingine kubwa ni Rais Samia kuunda kamati ikiwa ni sehemu kuongeza kasi katika utendaji kazi. Rais ameunda kamati ya haki jinai ambayo imetoa mapendekezo ya kuboresha utoaji wa haki kwa Watanzania.


Jambo lingine ambalo ni zuri, Watanzania watajivunia kurejeshwa kwa Tume ya Mipango. Ni hatari unaendesha nchi bila kuwa na mipango. Rais ameunda tume na wajumbe wameshateuliwa. Kwa mara ya kwanza, tume imeundwa kwa sheria ya bunge, hatua ambayo ni nzuri sana, hakuna mtu anayeweza kuja kuindoa tume hiyo kwa maneno tu.


Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jambo jema kuiweka Tume ya Mipango katika uendeshaji wa shughuli za uchumi. Jambo ambalo ni kubwa na muhimu lililofanyika ni nafasi ya sekta binafsi kuendesha uchumi wa taifa. Fursa hii ilitolewa mwaka 1987 wakati tunapobadilisha uchumi wetu kutoka uchumi dola kwenda uchumi huria.


Sasa sheria imetungwa na bunge ya PPP (Public Private Parternship), lengo ni kuongeza uwekezaji, ajira kwa Watanzania, hususani fursa za ajira kwa vijana wenye viwango tofauti vya elimu. Ukitoa nafasi kwa sekta binafsi kuwekeza, unakuza ajira na mapato kwa taifa.


Kete kubwa ni utekelezaji wa ilani ambapo tuna mkataba kati ya wapiga kura wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla, kama nilivyoeleza hapo awali.


SWALI: Katika kutekeleza dhana ya maridhiano, uliongoza timu ya viongozi wa CCM kufanya mazungumzo na CHADEMA, je, kuna tija yoyote iliyopatikana katika mazungumzo hayo?

 

JIBU: Rais amekuja na dhana ya maridhiano kwa nia njema kabisa. Lengo la maridhiano lilikuwa ni kudumisha umoja wa kitaifa, lengo la pili kukuza demeokrasia, lengo la tatu kuwa na umoja bila kujali tofauti zetu na lengo la nne ni kuimarisha amani na utulivu kwa sababu bila amani na utulivu maendeleo hayawezi kupatikana.

 

Ndivyo rais alivyotamka na nyie ni mashahidi alipotamka kupitia Baraza la Vyama vya Siasa, Kituo cha Demokrasia Tanzania. Rais akiwa ni Mwenyekiti wa CCM, kufungua milango kwa CHADEMA kilichokuwa na malalamiko mengi, kuanza maridhiano. Tumefanya vikao kwa zaidi ya mwaka na kusikiliza hoja. Je, maridhiano yameleta manufaa? Jibu ni ndiyo. Kamati mbalimbali zimetoa mapendekezo kadhaa juu ya namna ya kuimarisha demokrasia na mambo manne niliyoyataja hapo juu. Katika maridhiano tuliyoyafanya na CHADEMA, naweza kukiri tumeweza kutatua mambo mengi ambayo CHADEMA iliyaweka mezani. Nyinyi ni mashahidi ya kwamba wale viongozi wa CHADEMA waliokuwa nje, serikali ilitoa tamko warudi na wale waliokuwa na kesi zilifuatwa kwa taratibu na wengine waliokuwa na kesi, kesi zao zilifuata mkondo wa kisheria zikaondoka. Hii imedhihirika nia njema ya rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi.  

 

SWALI; Mwaka ujao ni mwaka wa uchaguzi mkuu, tayari wapo viongozi na wanachama wa CCM wametamka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndiye mgombea pekee wa nafasi ya urais katika kinyang’anyiro hicho, je, huku siyo kuminya demokrasia?

 

JIBU: Chama chetu kinaendeshwa kwa katiba, kinaendeshwa kwa kanuni, lakini vile vile kinathamini utamaduni wa chama chetu. Utamaduni wa chama chetu ni kwamba, rais anayemaliza muhula wake wa kwanza na anaenda muhula wa pili apewe ridhaa ya chama kuendelea kwa awamu hiyo. Huu ndio utamaduni tunaoendelea nao. Tumefanya hivyo kwa Rais Mkapa mwaka 1995 akaendelea hadi kwa 2005, tukafanya kwa rais Kikwete kwa muhula wa kwanza na wa pili, tukafanya hivyo kwa Rais Magufuli, muhula wa kwanza akamaliza tukaenda katika uchaguzi wa 2020. Sioni sababu kwa chama cha CCM kuachana na utamaduni huo. Kwanza ni utamaduni mzuri unaofanyika kwa kila kiongozi wa chama chetu. Ni utamaduni unaoimarisha umoja ndani ya chama chetu, tusingependa kufungua milango kutafuta mwingine na kutengeneza makundi yasiyokuwa na sababu maalumu.

 

Jambo la pili, kazi iliyofanywa na rais wetu ni ya kupigiwa mfano, hakuna kata au jimbo katika nchi hii hakuna shughuli ya maendeleo inayofanyika. Amefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na itakapofika 2025, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi utafika zaidi ya asilimia 100. Rais alipochukua uongozi alibeba dhamana ya kumalizia miradi yote aliyoikuta ikiwemo ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege, bwawa la umeme. Miradi hii inahitaji fedha nyingi; mambo yenye fedha nyinyi yanahitaji umakini na shughuli zote zinakwenda vizuri na zitamalizika chini ya uongozi wake kabla ya kuondoka madarakani. Bwawa la umeme sasa lina asilimia 90, alichukua uongozi likiwa na asilimia 30 na nina matumaini ndani ya muda mfupi tatizo la umeme litakwisha. Wana-CCM tuna kila sababu ya kumpitisha Rais Samia kugombea kwa awamu ya pili.

 

 

SWALI: Katiba ya Chama Cha Mapinduzi inatamka kwamba ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru; kutokana na mabadiliko ya mifumo duniani, je, itikadi ya ujamaa bado ina nguvu katika zama hizi?

 

JIBU: Mimi nataka niseme ni kweli kabisa chama chetu kilikuwa kinaweka msisitizo katika suala la ujamaa na kujitegemea, tafsiri hiyo bado ipo ikiwa ni falsafa. Muhimu ni kujali utu wa binadamu kuhakikisha jamii yote kuwa sawa na inapata heshima, inathaminiwa na inapata huduma sawa hiyo ndio tafsiri ya ujamaa.

Nadhani tukubali mambo haya ni lazima yaende na wakati. Ujamaa ni kuthamini utu wa mtu, usawa wa kila mmoja.

 

Suala la kujitegemea hili nadhani kila nchi inataka kujitegemea, Tanzania inataka kujitegemea, Marekani inataka kujitegema, Wajapani nao wanataka, Waarabu nao wenye mafuta, nao wanataka kujitegemea.  Katika dunia hii kila nchi inataka kujitegemea.

 

SWALI: Umesikika ukisema viongozi ama wa chama au serikali wanatakiwa kuwa “watumishi wa watu”, hii maana yake nini?

 

JIBU: Kila mtu anayechaguliwa na kila anayeteuliwa, nafasi anayokuwa nayo imetokana na ridhaa ya wananchi. Nafasi zote tulizokuwa nazo uwe kiongozi au mtumishi, zimetokana na umma.

Katiba yetu inasema mwenye mamlaka yote katika nchi hii ni wananchi. Hivyo mwananchi ndiye anayetuchagua na anatuweka madarakani. Nafasi zetu zinatokana na wao.

 

Ni muhimu kuwasikiliza, kuwa na mijadala nao. Na hapa nitawapa mifano, sasa tuna sera ya dira ya taifa na jijini Dodoma rais alianzisha mchakato na kuwataka wananchi kutoa maoni. Hii inaaminisha ni nini, maana yake ni kwamba viongozi na watumishi hawana hatimiliki ya kutekeleza mipango bila kuwashirikisha wananchi. Wananchi wana haki ya kusikilizwa na kustahili yale wanayoyataka yatekelezwe. CCM, viongozi na watendaji katika serikali tunatokana na wao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Abdulrahman Kinana

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages