LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 20, 2024

KATIBU MKUU LUHEMEJA AMKARIBISHA MKURUGENZI MKUU PSSSF, AAHIDI KUMPA USHIRIKIANO, KULIPA PENSHENI KWA WAKATI, UKAMILIFU NA USAHIHI

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja, leo Februari 20, 2024, amemkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Abdul-Razaq Badru, ambaye Februari 6, 2024, aliteulia hRais Dk. Samia Suluhu Hassan kungoza Mfuko huo.

Akimkaribisha katika kikao cha kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu huyo wa PSSSF, Mhandisi Luhemeja amezitaka taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo kuhakikisha zinatoa elimu juu ya kazi wanazofanya ili Wananchi waweze kuelewa vema majukumu ya taasisi hizo.

“Elimu juu ya taasisi zetu zote itolewe, haswa elimu ya Hifadhi ya Jamii iende kwa nguvu kwa wadau, naamini elimu ya Hifadhi ya Jamii ikieleweka vyema watu wengi hawatapoteza muda kwenye uwekezaji usio na tija” alisema Mhandisi Luhemeja.

“Ndugu zangu naomba muungane nami kumkaribisha Bw. Badru ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuongoza PSSSF, naomba tumpatie ushirikiano ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake, Bw. Badru hii ndio timu yako sasa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, karibuni sana", akasema Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Lumemeja alifurahiswa na kauli ya Bw. Badru kuwa mwelekeo wa utendaji lazima uendane na kusudio na lengo la uwepo wa taasisi husika.

“Kweli nimefurahishwa na hoja ya Bw. Badru, kwamba ili utendaji kazi uende vyema ni lazima mwelekeo ulenge kusudio na lengo la taasisi husika, hivyo kila mmoja wetu ni lazima ajue mwelekeo wa taasisi yake ili aweze kufikia malengo” alifafanua Mhandisi Luhemeja.

Kwa upande wake, Bw. Badru alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, ameahidi utendaji bora kwa kuzingatia miongozo na kanuni zilizopo.

“Kwa kweli nashukuru kwa kuwa sehemu ya timu hii chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, ninahidi ushirikiano kwenu ili kwa pamoja tuweze kutekeleza vyema majumu yetu” alisema Bw. Badru.

Bw. Badru alisema, PSSSF imejipanga kutekeleza vyema majukumu yake na kuendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama kwa kuendelea kutumia TEHAMA ili kila mwanachama afikiwe kwa wakati.

“Tutaendelea kutoa elimu mahususi kwa Wanachama ili waelewe zaidi juu ya PSSSF, tunahakikisha kila mdau atafikiwa na tunaahidi kulipa pensheni kwa wakati, ukamilifu na usahihi” aliahidi Bw. Badru.

Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Februari 6, 2024 alimteua Bw. Badru kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja, akizungumza wakati wa kumtambulisha Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). 
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru akizungumza baada ya kutambulishwa kwa kwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru (kushoto) akiwa pamoja na Bw.John Mduma Mkurugenzi Mkuu wa WCF na Bi. Khadija Mwenda, Mtendaji Mkuu wa OSHA wakifatilia hotuba iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mha. Cyprian Luhemeja, wakati akimtambulisha Bw. Badru.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages