LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 17, 2024

KATIBU MKUU CWT, WAJUMBE 9 WAKAMATWA NA JESHI LA POLISI

KATIBU mkuu wa chama cha walimu Tanzania (CWT) Japhet Maganga jana alikamatwa na jeshi la polisi mkoa wa Dodoma pamoja na wenzake 9 kutokana na sababu ambazo hazijawekwa wazi na viongozi wala wajumbe huku jeshi la polisi likiwa nalo halijaweka bayana chanzo cha kukamatwa kwake.


Tukio hilo lilitokea baada ya Rais wa CWT Leah Ulaya kumaliza kufungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye hoteli ya St Gasper Jijini Dodoma.


Baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa kikao hicho baadhi ya taarifa ambazo hazijathibitishwa na uongozi wa CWT au Jeshi la Polisi, baadhi ya wajumbe walieleza kuwa Katibu mkuu alisimama na kueleza kuwa licha ya Rais kufungua kikao lakini bado hana imani naye kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji jambo ambalo lilipelekea Rais wa CWT kupiga simu jeshi la polisi ili waweze kumkamata katibu huyo na kumweka ndani.


Chanzo hicho cha habari kinaeleza kuwa baadhi ya wajumbe waliotoa hoja ya kutokukubalina agizo la rais nao waliamriwa wakamatwe na kuwekwa ndani.


"Majira ya saa 4 asubuhi Katibu kasema kuwa hana imani na Mwenyekiti, rais alipiga simu polisi na kuingia kumkamata katibu,baada ya viongozi wote walioonesha kutoa hoja ya kupinga kukamatwa katibu nao waliamriwa wakamatwe"kilieleza chanzo hicho.


Licha ya kumkamata katibu mkuu wajumbe waliokamatwa ni

Khamisi Mmtundua,Mwenyekiti Mkoa wa Singida,Alfoncy Mbasa,katibu Mkoa wa Morogoro, Paulo Costan,Mwenyekiti Mkoa wa Kagera,Hamisi Chinahova Katibu Mkoa wa Mwanza, Aalen Shuli, Katibu Mkoa wa Shinyanga, Alistides Ishengoma,Mweka hazina Mkoa wa Mwanza, Mahanya Kyola,Idara ya Afya Makao Makuu, Filemon Leo ,Mwenyekiti Kyerwa na Daudi  Mafwili,Katibu Kilimanjaro.

HALI HALISI.

BAADA ya kumkamata Katibu Mkuu pamoja na wajumbe hali ya usalama iliongezeka kwa kiwango cha juu baada ya askali polisi waliovalia sale pamoja na waliovalia nguo za kiraia walionekana kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya viwanja vya ukumbi wa mkutano wa St. Gasper.


Hata hivyo bado uongozi wa CWT pamoja na jeshi la polisi halijaweza kusema lolote na ufuatiliaji ili kupata habari kamili unaendelea.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages