Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog
Hivi nani anaweza kusema hamjui Edward Ngoyai Lowassa? Hakuna. Na ikitokea yupo basi katika watu kumi atakuwa ni mmoja na wakizidi sana wawili, au mwenye rika la utoto. Kwa jumla jina la Lowassa linajulikana ndani na nje ya Tanzania.
Sasa ni kwa nini jina hili limekuwa alama isiyofutika katika kumbukumbu za kutunza majina ya watu? Ni kwa sababu Lowassa ambaye amefariki dunia leo Jumamosi, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam, amefanya mengi wakati wa uhai wake alioishi duniani kwa miaka 70.
Lowassa ambaye taarifa za kifo chake zimetangazwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amefariki akiwa amekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na changamoto za kiafya.
HUYU NDIYE LOWASSA
Kwa kuwa Lowassa amefariki akiwa ni Waziri Mkuu Mstaafu, tuanze na huo Uwaziri Mkuu. Ni kwamba alikuwa ni Waziri Mkuu wa kumi (10) wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishika nafasi hiyo Disemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kufuatia kuzongwa na sakata la kashfa ya Richmond iliyoibua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge hadi kuundwa Kamati ya kuchunguza sakata hilo.
Wakati wa sakata hilo la Richmond, Bunge liliamua kuunda Kamati ya kuchunguza sakata hilo na Dk. Harson Mwakyembe, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Spika wa Bunge wakati huo akiwa Samweli Sita ambaye ameshatangulia mbele za haki.
ALIKUWA NA HAZINA YA WAFUASI
Miongoni mwa mambo yanayofanya jina la Lowassa kubakia vichwani mwa watu wengi, ni kwamba Lowassa katika uwana siasa wake, alifanikiwa kuvuta wapenzi na mashabiki wake ambao walikuwa tayari kumsikiliza na kumfuata kokote alikokwenda.
Ni kwa sababu hiyo, pamoja na kujiuzulu Uwaziri Mkuu, lakini akaendelea kuzongwa na 'kashfa' ya ufisadi, lakini aliendelea kuwa mwanachama wa Chama Cha mapinduzi (CCM) kwenye utitiri wa wafuasi ambao waliomuamini na kumpigania katika kila jambo ndani na nje ya CCM.
Kwa kuamini kwamba bado ana mvuto kisiasa na ana wafuasi wengi wakati Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 unataradadi, aliingia katika harakati za kuwania kuombea urais kwa tiketi ya CCM, lakini katika mchakato wa ndani ya Chama hakufanikiwa baada ya jina lake kuondolewa na vikao vilivyokuwa vikichuja wagombea wa nafasi hiyo, akidaiwa kukiuka kanuni za maadili ya taratibu za michakato ya uchaguzi ndani ya Chama.
Baada ya kuenguliwa kuwa Mgombea baada ya CCM kumpitisha Dk. John Pombe Magufuli (sasa hayati) Lowassa alitamani kukata kiu yake au ya wafuasi wake, hivyo aliamua kuondoka CCM na kuingia CHADEMA ambako bila ajizi viongozi wa chama hicho kina Freeman Mbowe walimpa nafasi ya kugombea Urais kupitia CHADEMA.
Hakika, licha ya kuhamia ghafla Chadema, wakati wa uchaguzi huo wa urais mwaka 2015 Lowassa alikuwa na ushawishi mkubwa na hivyo kuleta upinzani mkubwa dhidi ya mgombea urais wa CCM, hata ikadhaniwa angewe kutwaa kiti. Lakini hakufanikiwa, maana katika matokeo ya Uchaguz yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi alishindwa kwa kupata asilimia 39.97 ya kura zote huku aliyekuwa mgombea wa CCM Dk. John Pombe Magufuli akipata asilimia 58.46.
Baada ya vuguvugu la uchaguzi mkuu kutulia, Lowassa baadaye alirejea tena CCM na kupokewa na Mwenyekiti wa CCM Rais Dk. Magufuli (hayati).
MAISHA YAKE.
Lowassa ni mwenyeji Monduli mkoani Arusha, aliyezaliwa Agosti 26, 1953 na baadae alifanikiwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo la Monduli na kuingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1990.
Lowassa alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, halafu shahada ya pili katika Sayansi ya maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.
Katika enzi za uhai wake Lowassa amepata nafasi ya kushika nafasi mbalimbali zikiwemo Uwaziri mdogo wa Mazingira na Mapambano dhidi ya umaskini katika Ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000).
Aliwahi pia kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa-AICC(1989-1990), Waziri mdogo wa Haki na Mambo ya Bunge katika ofisi ya Makamu wa Rais (1990-1993), Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990 na Disemba 2005 alipitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na ilipofika mwaka 2015 aligombea Urais.
Edward Lowassa enzi za uhai wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇