Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Zena Said, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo. 27 Februari 2024.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...
1. Naungana na walionitangulia kuzungumza kwa kumshukuru
Mungu aliyetuwezesha kushiriki katika Jukwaa
la Kodi na Uwekezaji la mwaka huu 2024. Nakushukuru Mhe. Dkt. Mwigulu
Nchemba (Mb.), Waziri wa Fedha, kwa kumualika Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mgeni Rasmi katika Jukwaa hili
muhimu. Mhe. Rais alidhamiria kushiriki nasi, lakini kutokana na majukumu
aliyonayo, amenipa heshima ya kumwakilisha. Vilevile, nawapongeza kwa dhati Mawaziri
wenye dhamana ya Fedha na Uwekezaji kutoka pande zote za JMT kwa kuratibu na
kuandaa Jukwaa hili kwa ushirikiano.
Waheshimiwa Viongozi na Washiriki wa Jukwaa;
2. Hapa Tanzania kuna mtizamo uliojengeka kuwa, mfumo wa kodi
umekuwa ni kikwazo katika uwekezaji na ufanyaji biashara. Hilo linathibitishwa na
kuwepo kwa malalamiko dhidi ya mfumo wa kodi kutoka kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji
- wa nje na wa ndani. Kwa mujibu wa taarifa
za Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Wafanyabiashara/Wawekezaji wamekuwa
wakilalamikia mambo kadhaa yakiwemo utitiri wa kodi, tozo na ada; Viwango vya
juu vya kodi, rushwa, makadirio ya kodi yasiyoakisi uhalisia, kutosomana kwa mifumo
ya kielektroniki katika taasisi za utoaji vibali, leseni na huduma nyinginezo;
kuwepo kwa sheria na kanuni zinazokinzana, na kuwepo kwa muingiliano wa
majukumu ya kitaasisi.
3. Serikali kwa upande wake, imekuwa ikilalamikia
kutozingatiwa kwa sheria na miongozo ya kodi na ukwepaji wa kodi unaofanywa na
baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji. Msingi wake ni kuwa Serikali yoyote, ,
inawajibika kulinda mipaka ya nchi, kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali
zao, pamoja na kujenga na kutunza
miundombinu mbalimbali. Kutokana na wajibu huo, Serikali inatoza kodi na kutafuta mikopo
na misaada kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa Serikali na utekelezaji wa
miradi ya maendeleo. Hivyo, wawekezaji na wafanyabiashara wasipolipa kodi
ipasavyo inadhoofisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake kwa umma. Serikali
pia ina jukumu la kutunga sera nzuri na kuweka mazingira bora yatakayowezesha
uwekezaji na ufanyajibiashara kushamiri na kuwawezesha walipakodi kutimiza
wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria. Ni vema kukumbuka kuwa, kwa
takriban muongo mmoja (2010/11-2022/23) makusanyo yetu ya kodi yamekuwa chini
ya 12% ya Pato la Taifa. Kiwango hicho ni chini ya wastani wa 15.6% kwa nchi za
Afrika. Hivyo, hatuna budi kuibua mikakati itakayotufikisha kwenye kiwango cha
kodi cha angalau 15% au zaidi ya Pato la Taifa. Nchi nyingi zilizo kwenye kundi
la kipato cha kati cha chini ziko juu ya 13%. Kwa mfano, Senegal 18.7%, Zambia
16.8%, Ghana 14.1%, Cote d’Ivoire 13.9% na Cameroon 13.3%.
4. Ni kwa muktadha huo, Serikali ya awamu ya sita tangu iingie madarakani imeendelea
kufanya maboresho ya sera, sheria na mifumo yetu
ya usimamizi wa kodi ili kujibu malalamiko ya Wawekezaji. Baadhi ya maboresho hayo,
ni yafuatayo:
·
Kurekebisha sheria za
kodi ili kutoa vivutio vya kodi kwa wawekezaji/wafanyabiashara wa kimkakati
chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC);
·
Kuweka utulivu wa sera
za kodi ambapo viwango vya Ushuru wa Bidhaa vinafanyiwa marekebisho kila baada
ya miaka mitatu (3) badala ya kila mwaka;
·
Kuendelea kujenga na
kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara ikijumuisha
ujenzi wa vituo 10 vya utoaji huduma kwa pamoja mipakani (One-Stop Border
Posts) ambapo vituo 6 vimekamilika na vinafanya kazi na vilivyobaki vinaendelea
na ujenzi na uwekaji wa mifumo ya TEHAMA;
·
Kufanya mapitio na
kuhuisha sera na sheria mbalimbali ili kuweka misingi mizuri na imara ya
kusimamia mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji;
·
Kuwianisha majukumu ya
kitaasisi ili kurahisisha utoaji huduma;
·
Kuendelea kufanya
mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la
Biashara (TNBC);
·
Kutoa vivutio vya
kikodi ikiwemo kutoa misamaha ya kodi na kiwango cha asilimia sifuri (0) cha
ushuru wa forodha kwa bidhaa mtaji na malighafi, zana za kilimo, ufugaji na
uvuvi; dawa za binadamu na mifugo na dawa zingine; vifaa vinavyotumika
kuunganisha mitambo na magari; na malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa
za dawa;
·
Kupandisha viwango vya
ushuru wa forodha kupitia Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ambapo hivi karibuni ilikubaliwa kiwango cha juu cha Ushuru wa Forodha kuwa
asilimia 35 ili kuhakikisha sekta za uzalishaji na za kimkakati zenye kuongeza
thamani katika malighafi na mazao ya ndani ya nchi zinalindwa kikamilifu dhidi
ya ushindani usio wa haki;
·
Kukamilisha Mfumo wa
Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuunganisha
mifumo ya taasisi saba (7) ambazo ni NIDA, TRA, BRELA, TIC, Kazi, Uhamiaji na
Ardhi. Hatua hii itawezesha huduma za usajili na uwajibikaji kwenye taasisi za
udhibiti na usimamizi kupatikana kwa haraka na wepesi zaidi; na
·
Kuanzisha Ofisi ya
Msuluhishi wa Malalamiko ya Walipakodi (Tax Ombudsman) ili kuharakisha
usuluhishi wa migogoro inayotokana na usimamizi wa sheria za kodi;
Waheshimiwa Viongozi na Washiriki wa Jukwaa;
5. Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kama nilivyozieleza kwa ufupi,
tumeanza kuona matunda mazuri na mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa
Tanzania ambayo yameimarika na kuwa bora zaidi katika kipindi kifupi cha uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan. Kuthibitisha hilo, Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na
nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Shahara, licha ya
misukosuko ya uchumi na kijamii inayoendelea Duniani kote. Katika mwaka 2023,
ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuwa 5.0% ikilinganishwa na 4.7% mwaka
2022. Matarajio kwa mwaka 2024 ni ukuaji wa 5.5%. Aidha, mfumuko wa bei
umeendelea kudhibitiwa ambapo katika
kipindi cha Julai hadi Desemba 2023 ulifikia wastani wa 3.2%, kiwango ambacho
kipo ndani ya lengo la kati ya 3.0% na 7.0% katika kipindi cha muda wa kati. Kwa
mujibu wa takwimu za TIC, jumla ya miradi 526 yenye thamani ya Dola za Marekani
5,720.36 Milioni iliandikishwa mwaka 2023 ikilinganishwa na miradi 256 yenye
thamani ya Dola za Marekani 3,749.32 Milioni mwaka 2021.
Sehemu kubwa ya miradi hii iliyoandikishwa TIC ilikuwa
kwenye sekta za Uzalishaji (Manufacturing), Ujenzi/Majengo ya Biashara,
Usafirishaji na Kilimo. Aidha, mikataba
mikubwa iliyosainiwa katika kipindi hicho ni pamoja na ununuzi wa asilimia 20 nyingine za hisa katika Kitalu cha Gesi cha Mnazi
bay zenye thamani ya dola za Marekani milioni 23.6 na Mkataba wa ubia na
kampuni ya Maurel and Promo (E&P); Mkataba
wa Makubaliano ya Msingi (Framework Agreement) baina ya Serikali ya Tanzania na
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Peak Rare Earth Limited ya Australia; Mkataba baina ya Tanzania na Kampuni Nne za
Madini za Black Rock Mining Limited, Strandline Resources Limited na Nyanzaga;
na Mkataba baina ya Serikali na Kampuni
ya DP World ya Dubai wa kuendesha shughuli kwenye bandari ya Dar es Saalam kwa
miaka 30. Taarifa za Mashirika
makubwa duniani yanayopima uwezo wa nchi kukopesheka (credit rating agencies)
yameiweka Tanzania katika nafasi nzuri. Mathalan, Taasisi ya Moody’s Investors
Service imeipa Tanzania alama ya B2 na Positive Outlook na
Taasisi ya Fitch imeipa Tanzania B+ na Stable Outlook. Kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali
kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaliongezeka kwa 22.1% kutoka Sh.
trilioni 17.6 mwaka 2020/21 hadi Sh. trilioni 22.6 mwaka 2022/23. Ongezeko hilo
la ukusanyaji wa mapato limeiwezesha Serikali kuendelea kuongeza Bajeti yake
kutoka Sh. trilioni 36 mwaka 2021/22 hadi Sh. trilioni 44.4 mwaka 2023/24.
6. Ongezeko la bajeti limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya
Kisasa (SGR) pamoja na injini na
mabehewa yake, mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (94.8%), mradi wa
Kinyerezi I Extension (100%) na mradi wa kufua Umeme wa Maji Rusumo (99.7%).
Vilevile, kupeleka huduma ya umeme kwenye vijiji 10,987 kati ya vijiji 12,318 vya
Tanzania Bara (sawa na 89.19%). Pia, ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali
ikiwemo ya barabara na madaraja unaendelea ambapo jumla ya miradi 23 ipo kwenye
hatua mbalimbali za utekelezaji, hii ni pamoja na daraja la Kigongo - Busisi
(80.0%), kuimarisha viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege mpya tano na kufanya
shirika la ndege kuwa na jumla ya ndege 14. Aidha, tunatarajia hivi karibuni kupokea
ndege nyingine mbili mpya aina ya Boeing 737-9 Max na Boeing 787 - 8
Dreamliner.
Waheshimiwa
Viongozi na Washiriki wa Jukwaa;
7. Kwa upande wa Usafirishaji kwa njia ya maji, ukarabati wa Meli ya MV. Umoja
umekamilika; ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza (Hapa Kazi Tu) unaendelea (93%);
ukarabati wa meli ya MV. Sangara unaendelea (92%); na kusainiwa kwa mikataba ya
ujenzi na ukarabati wa meli sita (6) zitakazojengwa katika Maziwa Makuu ukiwemo
mkataba wa ujenzi wa Karakana ya kujengea meli (shipyard) katika Ziwa
Tanganyika na mkataba wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba. Serikali pia,
inaendelea kuimarisha miundombinu ya bandari za Dar es Salaam na Tanga na
kuendelea na uimarishaji wa miundombinu katika bandari za Maziwa Makuu.
Vilevile, ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo eneo la Ruvu Mkoa wa Pwani
umefikia 96% ambayo inatarajiwa itaongeza ufanisi wa kuhudumia masoko ya nchi
jirani zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam.
8. Aidha, katika sekta ya kilimo Serikali imeendelea na ujenzi wa skimu za
umwagiliaji katika mikoa mbalimbali nchini; uanzishwaji wa mashamba makubwa yatakayokuwa
kitovu cha teknolojia bora kwa wakulima wadogo kupitia Programu ya Jenga
Kesho iliyo Bora (BBT); kutoa ruzuku ya mbolea na viuatilifu, kudhibiti
sumukuvu, ujenzi wa maghala 14 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 21,500 za nafaka katika mikoa 10 ili
kuboresha usalama wa chakula nchini.
9. Katika sekta ya Afya, Serikali imewekeza katika vifaa tiba, dawa, na rasilimali
watu katika ngazi mbalimbali. Uwekezaji mkubwa umefanyika katika eneo la
miundombinu kupitia ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya
kwa kuanzia Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum, Hospitali za Kanda, Hospitali
za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati katika Mikoa
yote nchini. Katika Elimu,
Serikali imeendelea na mpango wa kutoa elimu bila malipo na katika kipindi cha
Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais, ameongeza wigo wa elimu
bila malipo hadi elimu ya Sekondari. Aidha, Serikali imeendelea kutoa mikopo
kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu, imeboresha miundombinu ya kusomea, imepunguza
tatizo la upungufu wa walimu na imejenga Vyuo vya Ufundi katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na katika Wilaya 120 kati ya 184. Kwa upande wa Maji, vijiji 9,675 kati ya 12,319
vimeunganishwa na huduma ya maji safi na salama, sawa na takriban 79%. Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine katika sekta nyingine za uzalishaji
na kijamii kama vile uvuvi, madini, maliasili na utalii. Uwekezaji huu mkubwa
uliofanywa na Serikali ni mtaji mkubwa pia kwa Wafanyabiashara, Wawekezaji na
Wananchi kwa ujumla.
Waheshimiwa
Viongozi na Washiriki wa Jukwaa;
10. Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kusisitiza yafuatayo:
Jukwaa la Kodi na Uwekezaji ni fursa inayowakutanisha
wadau kutoka taasisi za umma na sekta binafsi ili kutoa maoni yanayolenga
kuboresha sera za kodi na uwekezaji nchini. Utaratibu huu ni mzuri kwani
unaimarisha ushiriki wa wadau katika kuboresha sera za kodi na uwekezaji ikiwa
ni maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25. Katika hotuba yake Mhe.
Waziri wa Fedha ameeleza kuwa sehemu kubwa ya maoni yaliyotolewa kwenye Jukwaa
lililopita yalizingatiwa katika mchakato wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/24.
Hivyo, nawaomba washiriki wote kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru ili tuweze
kuboresha zaidi sera zetu za kodi na uwekezaji nchini. Napenda kuwashawishi
kwamba michango yenu ijielekeze katika kuibua njia za kibunifu zitakazosaidia
kuongeza mapato ya Serikali bila kuumiza Wafanyabiashara na Wawekezaji. Jadilianeni kwa kina kuhusu namna ya kutumia zaidi ubia kati ya sekta ya umma na sekta
binafsi, mathalan kupitia hatifungani zitakazotolewa na taasisi na mashirika ya
umma kugharamia miradi ya maendeleo.
Itafaa pia mjadala wenu ujielekeze katika kubaini na kudhibiti
vihatarishi vya matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali,
ikiwemo wizi wa kimtandao na utoroshaji wa mitaji (capital flight). Ninaamini
pia kuwa Jukwaa hili litaibua mbinu za kuvutia uwekezaji zaidi nchini ikiwemo
nafasi ya kuingia mikataba ya kuepuka utozaji wa kodi mara mbili. Ni vema pia endapo
Jukwaa hili litapata nafasi ya kujadili kuhusu uwezeshaji na vivutio kwa
wawekezaji wa ndani bila kuathiri ubora wa bidhaa na ushindani. Mwisho, ningependa kuliachia Jukwa hili
changamoto ya kubainisha jinsi ambavyo falsafa ya Mhe, Rais ya 4R ( Reform,
Rebuilding, Resilience & Reconciliation) inavyoweza kutumika kuakisi mfumo
wa kodi na mazingira ya uwekezaji nchini ili kuweza kufikia ndoto yetu ya kuwa
nchi ya kipato cha kati cha juu au zaidi ifikapo mwaka 2050.
Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
JMT napenda kutamka kuwa “Jukwaa la kodi
na uwekezaji kwa ajili ya maandalizi ya bajeti kwa mwaka 2024/25 limezinduliwa
rasmi”.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇