LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 2, 2024

WAKATI TET IKIRINDIMA MOROGORO KUWANOA WAWEZESHAJI NA WALIMU SHULE BINAFSI KUKABILI MITAALA ILIYOBORESHWA, WIZARA YAMSHUKURU RAIS DK. SAMIA

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog, Morogoro
Wakati Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ikianza kurindima kuwanaoa wawezeshaji na walimu wa shule binafsi kukabili mitaala iliyoboreshwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia serikali ya Awamu Sita anayoongoza, kwa maboresho makubwa yanayoendelea katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu lengo likiwa kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu iliyo bora.

Shukurani hizo za Wizara hiyo zimetolewa na Katibu Prof. Carolyne Nombo, wakati akifungua Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wawezeshaji na Walimu wa shule binafsi, waweze kuikabili vema mitaala iliyoboreshwa, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kufanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B mjini Morogoro, leo Januari 2, 2024.

Kuhusu mafunzo hayo Prof. Carolyne alisema Serikali imeidhinisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 pamoja na Mitaala iliyoboreshwa ya mwaka 2023, hivyo kuidhinishwa kwa mitaala kumeleta uhitaji wa mafunzo kwa wasimamizi na watekelezaji wote wa mitaala hiyo.

Alisema, mifano mbalimbali duniani inaonesha ujenzi wa mfumo bora wa elimu unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa walimu wanaouendesha hivyo ni wazi ili mabadiliko yoyote ya sera na mitaala ya elimu yaweze kuleta tija iliyokusudiwa ni lazima walimu waandaliwe vema.

"Aidha, ili mitaala itekelezwe kwa ufanisi, ni lazima kuwe na walimu wenye weledi, maadili na ari stahiki, kwa kulitambua hili, Serikali imejipanga kutoa mafunzo ya walimu kazini kwa walimu wote wa shule za umma na zisizo za Serikali ili kuwawezesha kuielewa mitaala iliyoboreshwa na kuitekeleza kwa ufanisi", alisema Prof. Carolyne.

Alisema mafunzo hayo yatasimamiwa na TET ambayo tayari imeandaa wawezeshaji wa kitaifa wakiwemo wahadhiri kutoka katika vyuo vikuu vya umma na binafsi, Wakufunzi wa Vyuo vya Serikali na visivyo vya Serikali, Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa Elimu Kata na hadi sasa wawezeshaji 10,557 wa Kitaifa wameshawezeshwa kuweza kutoa mafunzo husika katika maeneo zilizopo shule zote.

"Kutokana na uhitaji mkubwa wa mafunzo na idadi kubwa ya walimu inayohitaji kuwezeshwa, Serikali kupitia TET imeona ni vyema kuongeza namba ya wawezeshaji wa kitaifa kutoka katika kundi la shule zisizo za Serikali na hili ni moja ya makubaliano ya kikao kati ya Serikali na viongozi wa taasisi mama zinazosimamia shule zisizokuwa za serikali (umbrella organisations) kilichofanyika Disemba 29, 2023.

Nimejulishwa kuwa katika kikao chenu mlikubaliana kuwa taasisi mama zitaletawashiriki  mahiri kumi watakaowezeshwa na TET na kuwa washiriki hawa watasaidia kwenda kujenga uwezo kwa walimu wengine wa shule zisizo za Serikali, ni kwa msingi huo pia TET imeona ni vema itumie fursa hiyo pia kuwawezesha walimu wote wa shule zisizo za Serikali katika Manispaa ya Morogoro", " alisema Prof. Carolyne.

Prof. Carolyne alizipongeza taasisi mama kwa kukubali kushirikiana na Serikali katika kuongeza idadi ya wawezeshaji watakaoendelea kutoa mafunzo haya kwa walimu na kuwashukuru pia kwa kuwagharamia washiriki kutoka katika taasisi hizo na kuwezesha upatikanaji wa eneo linalotolea mafunzo hayo.

Pia aliwapongeza washiriki waliohudhuria mafunzo hayo, akisema ana matumaini kuwa watatumia fursa hiyo muhimu kushiriki kikamilifu kwa muda wote wa mafunzo kwa ajili ya  kujiandaa vyema kutekeleza mitaala kwa umahiri na kufanikisha lengo la Serikali la kuboresha elimu nchini.

"Ninapenda kusisitiza kuwa mafunzo kwa walimu wa shule zisizo za Serikali yasiendeshwe kama biashara kwa kuwalipisha walimu. Wawezeshaji kutoka shule zisizo za Serikali mtawezeshwa kama nilivyosema, lakini hamtaruhusiwa kwenda kufanya biashara ya mafunzo kwa walimu juu ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR-TAMISEMI kupitia Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa Elimu Kata watafuatilia kuhakikisha kuwa walimu wa shule zisizo za Serikali hawatozwi fedha za mafunzo, ili kuhakikisha mafunzo haya hayachangishwi, Serikali kupitia Wizara itatoa mwongozo utakaoweka bayana kuwa mafunzo haya ni bure kwa walimu wote na kuwa mwalimu hatatozwa chochote," alisema Prof. Carolyne.

Ili kufanikisha hilo, Prof. Carolyne. aliiagiza TET kuendelea kufanya uratibu wa mafunzo yote yanayohusu utekelezaji wa mitaala kwa kushirikiana na taasisi mama za shule zisizo za Serikali, na kamwe  mawakala wasitumike katika kuratibu au kutoa mafunzo hayo.

Alisema, Ili kuhakikisha Serikali inapata taarifa na ufuatiliaji wa mafunzo hayo anaielekeza TET kuratibu mpango mzima wa utoaji wa mafunzo, kukusanya takwimu zote muhimu na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mafunzo.

"Naomba pia kusisitiza kuwa sualala Mafunzo ya Walimu Kazini ni la lazima na siyo hiari kwa walimu wote nchini wa shule za umma na shule zisizo za Serikali, hivyo, hata baada ya mafunzo haya tuendelee kujenga umahiri wa walimu kwa kupitia utaratibu wa mafunzo endelevu ya walimu kazini yaani MEWAKA.

Kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo haya, nimatarajio yangu kuwa wote mnaoshiriki mafunzo haya mtayafuatilia kwa umakini ili yalete matokeo chanya katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kwa kufanya hivyo mtakuwa mmesaidia kuiwezesha Serikali kufikia azma yake ya kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wa elimu nchini", alisema Prof. Carolyne.

TET
Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba alisema utoaji wa mafunzo hayo umefanyika kufuatia kukamilika kwa kazi ya uboreshaji wa mitaala ya elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu ambako kumeleta uhitaji wa kuwawezesha walimu kufahamu maboresho yaliyofanyika ili waweze kutekeleza tendo la ujifunzaji na ufundishaji kwa kadiri ya matarajio ya mitaala.

Alisema, mafunzo hayo yaliyoanza leo yatatolewa kwa siku tatu kwa makundi mawili ya wawezeshaji na walimu wa Darasa la Awali na Elimu ya Msingi wanaofundisha shule zisizo za serikali na kwa idadi yatahusisha wawezeshaji 163 na walimu 600 jumla ni 763.

Dk. Aneth alisema lengo kuu la Mafunzo kwa wawezeshaji ni kuongeza idadi ya wawezeshaji wa Kitaifa smbao watashirikiana na TET katika kutoa mafunzo kwa walimu wote wa darasa la Kwanza mpaka la Sita. Kwa hiyo baada ya mafunzo haya inataraajiwa kutakuwa na wawezeshaji wengi kutoka shule za
serikali na sisizo za serikali.

"Aidha, lengo la mafunzo kwa walimu wa Darasa la Awali na Elimu ya Msingi ni kuwawezesha kuhusu mambo
mbalimbali ikiwemo maboresho mahsusi ya mitaala yaliyofanyika ambapo washiriki watapitishwa katika Muundo wa Elimu, Dira na malengo makuu ya Elimu nchini, Malengo ya Elimu ya Awali na Msingi, Maeneo ya Ujifunzaji, umahiri na masomo katika ngazi ya elimu ya awali na msingi mtawalia.

Kwa Mfano maeneo ya ujifunzaji ya Elimu ya Awali yameboreshwa na sasa ni matano kama ifuatavyo:
•Utamaduni, Elimu ya Imani, Sanaa na Michezo, • Lugha na Mawasiliano, • Stadi za awali za maisha, • Afya na Mazingira, • Stadi za awali za Kihisabati, Kisayansi na TEHAMA.

Aidha, maeneo ya ujifunzaji kwa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza na la Pili nayo yameboreshwa na sasa ni matatu ambayo ni Lugha, mawasiliano na stadi za hisabati, Utamaduni, Imani Sanaa na michezo pamoja na Afya na Mazingira", alisema Dk. Aneth na kuongeza;

"Kwa upande wa Darasa la 1-6 maeneo ya ujifunzaji ni matano ambayo ni Lugha na mawasiliano, Hisabati, Sayansi ya Jamii, Sayansi na Teknolojia na Sanaa na Michezo".

Dk. Aneth alifafanua kuwa, maeneo hayo katika ngazi ya Elimu ya Msingi Darasa la 1- 6 yamebeba masomo ya Kiswahili, Kiingereza lugha za kigeni za Kiarabu, Kichina na Kifaransa, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili, Jiografia na Mazingira, elimu ya Dini, Sayansi na Sanaa na Michezo.

Alimwambia Katibu Mkuu kwamba Washiriki pia watachambua Mtaala wa elimu ya Awali na Msingi pamoja na Muhtasari wake kuwawezesha kujifunza juu ya utekelezaji wa mitaala katika ngazi ya darasa.

"Mfano watapitishwa juu ya muda wa utekelezaji wa mtaala kuanzia muda wa kipindi mpaka
saa na siku ambazo zinatakiwa katika kutekeleza mtaala kwa mwaka na kwa ngazi husika. Kwa mfano mtaala wa elimu ya awali unasema kuwa Mwaka wa masomo una siku 194 sawa na wiki 39 zenye mihula miwili ya masomo.

Muda wa ujifunzaji kwa siku ni saa tatu na nusu na muda wa kipindi ni dakika ishirini. Hivyo mtaala unabainsiha muda wa Vipindi vya masomo na muda wa kufanya shughuli nyingine za ujifunzaji ikiwemo kucheza, kujisomea na kupumzika", alifafanua Dk. Aneth.

Alisema pia washiriki watapitishwa katika mambo kadhaa ikiwemo (i) Namna ya Kuchopeka matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa kila umahiri na masomo, (ii) Kutumia teknolojia na kufaragua zana katika ufundishaji na ujifunzaji. (iii) Kuchopeka masuala mtambuaka mbalimbali katika Masomo Bebezi.

Alitaja baadhi ta Masuala mtambuka yaliyochopekwa katika ngazi ya Elimu ya Awali na msingi kua ni;
Mazingira,  Afya, Elimu jumuishi, Elimu ya jinsia, Elimu ya ya Amani na maadili, Haki na wajibu wa mtoto, Haki za binadamu, Ulinzi na usalama, Usalama barabarani, Elimu ya fedha, Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na Ushirika na masuala ya muungano.

Dk. Aneth alisema, baada ya mafunzo hayo kwa wawezeshaji kukamilika jukumu la taasisi mama litakuwa kuratibu uaandaaji wa mafunzo kwa walimu wa shule zao katika ngazi za mikoa, Kanda au Halmashauri na zitatoa ratiba ya mafunzo hayo kwa TET itakayobainisha tarehe, ukumbi na muda wa mafunzo husika ili kuiwezesha TET kuratibu na kusimamia utoaji wa mafunzo hayo.

"Na jambo hili ni mojawapo ya makubaliano yaliyotolewa katika kikao kati ya serikali na taasisi hizi. Hivyo
TET itasubiri ratiba husika na tumejipanga kusimamia na kuhakikisha kuwa mafunzo ya mtaala ulioboreshwa yanawafikia walimu wote wa shule za Umma na Binafsi na yanawawezesha kutekeleza mitaala kwa usahihi.

Taasisi zilizotoa washiriki wa mafunzo hayo ni Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii Tanzania (CSC), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Tanzania Association of Private Investors (TAPIE), Baraza la Sunnah Tanzania (BASUTA), Mrtandao wa Elimu Tanzania (TENMET).

Nyingine ni Tanzania Association of Women Owners of School and Colleges (TAWOSCO), Umoja wa Wazazi wa CCM Tanzania, Tanzania School Empowerment and Service Organiation (TASESO), Shule za Wasabato na Shule za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Wawezeshaji na Walimu wa shule binafsi, waweze kuikabili vema mitaala iliyoboreshwa, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kufanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B mjini Morogoro, leo Januari 2, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, kufungua Mafunzo hayo ambapo kabla ya kumkaribisha alieleza kwanza lengo na maudhui ya mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Mitaala TET Dk. Fika Mwakabungu, akimkaribisha Katibu Mtendaji wa TAPIE Laurent Gama kutoa neno la shukurani.
Katibu Mtendaji wa TAPIE Laurent Gama akitoa neno la shukurani.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa 'wamefurika' ukumbini.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa 'wamefurika' ukumbini.
Wawezeshaji wakiwa tayari kwenye mafunzo hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba (kulia) baada ya kufungua mafunzo hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo akizungunza nje ya ukumbi na wawezeshaji wa mafunzo hayo, baada ya kuyafungua. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Mitaala TET Dk. Fika Mwakabungu na wapili ni Mwenyekiti wa Umoja wa Waanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Dar es Salaam Mwajabu Mbwambo.
Mkurugenzi Mkuu TET Dk. Aneth Komba akizungumza na Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Mwajabu Mbwambo, nje ya ukumbi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages