Zanzibar
Msajili wa Hazina Tanzania Bara Nehemiah Kyando Mchechu na Msajili wa Hazina wa Zanzibar Waheed Muhammad Ibrahim Sanya wamekubaliana kuongeza weledi katika kusimamia mashirika kwa manufaa ya umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi hao pia wamekubaliana kubadilishana wafanyakazi na uzoefu wa utendaji wa kazi kitaalam, huku wakisisiza kuwa kioo cha ufanisi wa utendaji kazi na kushiriki kikamilifu katika kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar
Hayo yamejiri katika mazungumzo baina ya Mchechu na Sanya, Mchechu alipotembelea Ofisi ya Msajili wa Hazina Zabzibar, jana, Januari 11, 2024, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa 'Memorandum of Understanding' iliyotiwa saini April, 2023, kati ya ofisi hizo mbili.
Makubaliano hayo yana lengo la kuijengea uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar katika kusimamia Mashirika ya Umma kwa kutumia uzoefu wa muda mrefu wa ofisi ya msajili wa Hazina Tanzania Bara iliyoanzishwa mwaka 1959.
Hadi sasa ina mashirika zaidi ya 300 katika sekta mbalimbali za kibiashara na zile huduma wakati Ofisi ya Msajili Zanzibar ikiwa kwa sasa inasimamia mashirika yapatayo 17 tangu ilipoanzishwa mwaka 2021.
Ofisi hiyo imejipanga kuhakikisha mashirika hayo 17 yanaleta tija kulingana na malengo ya kukuza uchumi kulingana na maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi.
Lengo la Ofisi hizo ni kuweka msukumo wa kuyafanya Mashirika ya Umma yawe na ufanisi iuliokusudiwa yachochee uchumi katika Serikali zote mbili.
Pamoja na ziara ya kikazi, Mchechu pia yupo visiwani Zanzibar kushiriki katika maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo kilele chake ni leo Januari 12, 2024.
Msajili wa Hazina Tanzania Bara Nehemia Mchechu na Msajili Hazina Zanzibar Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, wakiwa katika mazungumzo katika Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, mjini Zanzibar jana.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇