NA VICTOR MAKINDA, MOROGORO
Chama Cha Mapinduzi
CCM, Wilaya ya Morogroro mjini Mkoani Morogoro, kimesema kuwa kimefurahishwa na
uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumteua Balozi
Dkt Emanuel Nchimbi kuwa katibu Mkuu wa chama hicho, uamuzi ambao pia
umeridhiwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kwa kuwa Dkt Nchimbi licha ya uweledi wake katika uga wa uongozi,
anakijua vyema chama hicho.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Morogoro mjini,
Fikiri Juma (anayeongea pichani), wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
mjini Morogoro kwa lengo la kuelezea namna chama hicho kinavyosimamia
utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020.
Fikiri alisema kuwa
CCM imefanya chaguo sahihi kwa wakati sahihi kwa kumteua mtendaji mkuu wa chama
aliyekulia ndani ya chama na anayekijua
vyema chama hicho hivyo anao uwezo mkubwa wa kuendelea kukijenga na kukitetea
chama kwa nguvu ya hoja hususani kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye
uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani
2025.
“Uteuzi wa Dkt Nchimbi
kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama, umepokelewa vizuri na Watanzania
wote, sisi wana CCM wa wilaya ya Morogoro mjini tunaungana na watanzania
wenzetu kumpongeza kwanza Mwenyekitiwetu wa chama Taifa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Kamati kuu (CC) na Halmashauri Kuu
(NEC) kwa uteuzi huo makini ambao umelenga kuendelea kukipa nguvu chama chetu
na kukifanya kiendelee kuaminiwa na watanzania “ Alisema Fikiri.
Fikiri aliongeza
kusema kuwa historia ya uongozi wa Dkt
Nchimbi ndani ya CCM na serikalini haiacho doa kwani amekuwa ni kiongozi mpenda
haki na maendeleo huku akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu
za kazi, hivyo anaamini kuwa uongozi wake ndani ya CCM, utakuwa na tija kubwa
kwa chama hicho.
“Sifa ya usikivu, ukomavu wa kisiasa, uanadiplomasia na
uwepesi wake wa kuelewa na kujibu hoja kwa kutumia nguvu ya hoja na sio hoja ya
nguvu ni sifa ambazo Dkt Nchimbi amejaaliwa nazo ambazo zinatutia matumaini
makubwa wana CCM wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuwa chama chetu kitazidi
kuwa imara.” Anasema Fikiri
Fikiri anaongeza
kuwa Dkt Nchimbi amepitia Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM) na amekuwa
mwenyekiti wa umoja huo na nafasi nyingine nyingi ndani ya chama hicho kikongwe
Afrika, hivyo anaamini kuwa amepikwa vya
kutosha kuwa kiongozi mahiri kwa kuwa UVCCM ni tanuru la kupika viongozi mahiri.
Akizungumzia kuhusu
utekelezaji wa ilani ya CCM wilaya ya Morogoro, Fikiri anasema kuwa chama hicho
kinajivunia kwa jinsi kilivyofanikiwa kutekeleza ilani ya chama kwa kiasi
kikubwa wilayani Morogoro.
“Ninampongeza Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz
Abood, baraza la Madiwani Manisapaa ya Morogoro na watendaji wa serikali wa
nafasi mbali mbali kwa kufanya kazi kwa bidiii kuhakikisha wananchi wa Morogoro
mjini wanaondokana na kero za maji, umeme, huduma za afya, elimu na ubora wa
shughuli za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na biashara.” Anasema.
Anasema kuwa Manispaa ya Morogoro imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za jamii na maisha ya wakazi wake kwa kuwa CCM imejidhatiti kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇