LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 25, 2023

SIO LAZIMA UKIISHIA LA 7 USIWE NA FAIDA KWA WENGINE

Na Yahya Msangi, Togo

Ukiwasikiliza waliokataa shule kama Salvatory Mkami, Uhuru Fundisha, Hillary A Silayo, Dutta Sagwa na Abubakari Zuberi, utadhani ni waliosoma tu ndio wanatakiwa wasaidie jamii. 


Hawaelewi kuwa hata wao japo waliwinda tetere wenzao wakiwa darasani wanatakiwa wawe na msaada kwa jamii. Lakini wao kutwa kucha kulalamikia wasomi. Yaani wanadhani wao wanatakiwa wasaidiwe tu kana kwamba ni tumbili shambani kwa mkulima.😀


Leo nataka nikupe kisa cha kweli kuhusu mtu ambaye hakusomea fani ya udaktari na alikuwa na elimu ya sekondari tu lakini ndiye aliyeasisi taaluma ya upasuaji moyo. 


Kijana huyu alikuwa Mmarikani mweusi akiitwa Vivian Thomas. Alipomaliza sekondari Vivian alitamani sana awe daktari. Siku moja akaenda hospital maarufu ya John's Hopkins. Iko pale Baltimore Maryland. Na ukifika kwenye ukumbi utaona kuna picha yake chini imeandikwa Dk. Vivian Thomas, PhD. Sasa ni marehemu (1940-1985) lakini hakuwahi kusomea udaktari. Alipewa tu udaktari. Udaktari wake sio ule wa 'heshima'. Alipewa udaktari kamili. 


Basi kijana huyu siku moja alienda pale hospital akaomba kuonana na daktari bingwa wa upasuaji akiitwa Dr. Alfred Blalock (1899 - 1964). 


Akamwambia dokta "nataka niwe msaidizi wako". Dr Alfred akaona kama mzaha. Ila akamkaribisha kwenye maabara yake.


Wakati huo Dr. Alfred alikuwa na mgonjwa; alikuwa mtoto wa miezi kama 3 hivi. Akisumbuliwa na tatizo la moyo. Pale maabara alikuwa ana mchoro wa moyo akijaribu kutafiti namna anavyoweza kumfanyia yule mtoto upasuaji. Wakati anaendelea kuchunguza ule mchoro Vivian akamwambia "nadhani tukikata hapa, tukatoboa hapa, tuka.... hili tatizo linaweza kutibika"!


Dr. Alfred akaduwaaa! Akaona kama kuna ukweli. Lakini alipowaeleza madaktari bingwa wenzake wakamwambia "ukifanya hivi utamuua mtoto"! 


Dr. Alfred akaingia wasiwasi. Vivian akamwambia usihofu. Tujaribu. Kabla ya operesheni Dr. Alfred akaandaa tafrija nyumbani kwake ili ajaribu kuwashawishi wenzie. Akamualika na Vivian. Ila Vivian akapangiwa kazi ya kuhudumia wageni vinywaji. Na wageni wakamdharau sana. Alikuwa ndiye mweusi pekee kwenye  tafrija. Hili lilimsononesha Vivian. Akataka aache kazi. Mkewe akamshauri asiache. 


Akarudi kazini. Lakini mshahara wake ulikuwa mdogo sana maana hakuwa kasomea udaktari. Kila Dr. Alfred akijitahidi wamuongezee wenzake wanapinga. Umuongezee kilaza? Vivian akapitia manyanyaso mengi. Leo nayaweka kiporo kama cha mwamedi dai uji.


Ikafika siku ya operesheni. Pale Hopkins chumba Cha upasuaji kina viti kama ukumbi wa sinema. Wapasuaji wanakuwa chini madaktari na wanafunzi wa udaktari wanatizama. 


Bado kulikuwa na upinzani mkali dhidi ya Ile operesheni. Mpaka mama na baba wa yule mtoto waliingia hofu. Ila Dr. Alfred akawaambia "bila operesheni atakufa na operesheni anaweza afe au apone chagueni"! Wakachagua operesheni. 


Wakati operesheni inataka kuanza Dr. Alfred akaenda kumchukua Vivian. Astaghifulah! Watu hooo huyo sio doktaaaa, huyo kima mweusiiiii, utasababisha hospital idharauliweeee, ! Dr. Alfred akamwambia Vivian "haya Bismillah"!


Wakampasua mtoto huku Vivian akiongoza zoezi! Watu wameduwaaa. Wazazi wa mtoto hoiii!


Baada kama ya saa 3 mtoto akazinduka na kutabasamu. Ukumbi ukalipuka kwa nderemo. Hii ndio ikawa operesheni ya kwanza ya moyo (first heart surgery) duniani. Inaitwa "BLUE BABY OPERATION". Blue kwa kuwa rangi ya mtoto haswa macho iligeuka kuwa ya blue kutokana na tatizo la moyo. 


Operesheni hii iliweka msingi wa operesheni zilizofuatia duniani kote. 


Kutokana na operesheni hii ndio Vivian akatunukiwa PhD kamili. 


Sasa nyie vijana ambao shule iligoma msikae kulaumu wasomi. Hata nyie mnatakiwa msaidie jamii. Sio kusoma ulikwepa, kazi kulaumu, kuhudhuria mikutano ya kijinga,  kuandamana na kukaa barabarani. Unaamini utasaidiwa na wasomi.

Muigeni Vivian.

Yahya Msangi

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages