Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali kabla
ya kuzindua Mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050. Rais Samia alifanya uzinduzi huo wakati wa Maadhimisho
ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano
wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Rais Samia akibofya kwenye kompyuta ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kuanza kwa mchakato huo.
Na Richard Mwaikenda, Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa matarajio ya Dira inayoandikwa ni kuweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula kwa ajili ya bara la Afrika na kwingineko duniani.
"Dira mpya itakayoandikwa, itilie maanani kwamba Dunia inakabiliwa na uhaba wa kutokuwa na usalama wa chakula. Matarajio ya Dira inayoandikwa ni kuweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula kwa ajili ya bara la Afrika na kwingineko duniani," amesema Rais Samia.
Amesema Katika kilimo, nchi imefanya kazi nzuri, sasa Tanzania inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 na huku tukielekea asilimia 140 ifikapo mwaka 2025.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa uzinduzi mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika sambamba na Maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma Desemba 9, 2023.
Akizungumzia upande wa elimu,Rais Samia amesema kuwa Dira ya 2020-2025, ilitaka kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ya msingi. "Tumefanikiwa kukamilisha lengo hilo, pia watoto wanaenda mpaka kidato cha nne bila malipo."
Amesema licha ya ongezeko na kuimarika kwa miundombinu ya elimu na wahitimu, bado kuna haja ya kuongeza hadhi ya elimu inayotolewa, hivyo Dira mpya ni lazima ielekeze kujibu maswali yanayohusu elimu yetu na mchango wake katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Nchi yetu ina miradi ya aina mbalimbali inayotekelezwa, ni imani yetu kwamba itakapofika mwaka 2025, yale malengo tuliyowekewa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2020-2025 tutayakamilisha." amesisitiza.


No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇