Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog, Dar es Salaam
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulianzishwa na Serikali kwa Sheria ya Bunge nambari 11 ya mwaka 2006 Sura ya 422, kwa lengo la kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwenye maeneo yaliyosalia kufikiwa mijini na maeneo mengi yaliyo mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma ya mawasiliano,
Kutokana na umuhimu huo, Mwaka 2009, kanuni za kuhuisha Mfuko huo, zilipitishwa na ukaanza kazi Julai Mosi, 2009.
Mfuko huo pia unayo dhamana ya kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi na za umma katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wote katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu, sanjari na kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hayo hafifu.
Pia UCSAF ina dhima ya kutengeneza mfumo kwa ajili ya upatikanaji wa mitandao ya mawasiliano na huduma rahisi na zenye ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji katika soko la kiushindani, kuhamasisha utoaji wa huduma bora katika viwango nafuu na kuhakikisha kuwa teknolojia ya habari na mawasilianpo inapatikana vijijini na sehemu za mijini kwa gharama nafuu, kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa wote kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kupitia ushiriki wa sekta binafsi.
Miongoni mwa kazi ilizopewa UCSAF pia ni kubaini maeneo ya miradi ya mawasiliano yanayoweza kupata ruzuku kutoka katika Mfuko huo, kuweka vigezo vya utambuzi wa maeneo ya vijiji vinavyohitaji na ambavyo haviwezi kupata huduma ya mawasiliano kwa sababu ya kutokuwa na mvuto wa kibiashara, kuweka vigezo sahihi vya utoaji wa ruzuku kwa watoa huduma za Mawasiliano kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo yaliyoainishwa.
Mfuko pia una jukumu la kutathmini miradi ya mawasiliano inayowasilishwa na watoa huduma ili kupewa ruzuku na Mfuko, kufanya tafiti mbalimbali na kufuatilia maendeleo ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yale yasiyo na mvuto wa kibiashara, kuishauri Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusiana na mambo yanayohusu Mawasiliano kwa wote.
Kuangalia njia sahihi za kutoa ruzuku kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini na katika maeneo yasiyo na mvuto kibiashara, kusimamia kisheria mikataba ya utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wote, kuweka utaratibu mzuri wa kusimamia, kukokotoa na kukusanya tozo za Mawasiliano kwa wote kutoka kwa watoa huduma, kukokotoa, kupanga na kugawanya ruzuku za mawasiliano kwa wote.
Sanjari na majukumu hayo yote, Mfuko huo unayo majukumu ya kupendekeza sera madhubuti za Mfuko kwa Waziri wa Sekta ya Mawasiliano, kushauriana na Kushirikiana na Wizara za Serikali, Idara au Mamlaka inayojitegemea kuhusiana na masuala ya huduma kwa wote.
Ikiwa majukumu hayo ndiyo malengo ya serikali kuanzisha Mfuko huo, je, sasa Mfuko umeweza kukidhi kiu ya Serikali hasa hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuhakikisha huduma za Mawasiliamo zinamfikia kila Mtazania?
Wakati wapo wanaoweza kukiri kwamba hakika UCSAF imekidhi kiu, lakini pia wapo ambao hawakiri hilo na sababu kubwa itakuwa ni kwa kuwa hawajapata fursa ya kujua yanayofanywa na yanayoendelea kufanywa na Mfuko huo.
Mimi ni miongoni mwa waliokuwa hawajui vilivyo kwamba kwa muda mrefu tayari UCSAF imeshafanya mambo makubwa ambayo kila anayeyajua bila shaka ataupa kongole Mfuko huo, na kukiri kwamba, hakika serikali ilifanya jambo sahihi kuutunga Mfuko huo.
Leo Jumanne, Novemba 21, 2023 ndiyo nimepata kuyajua vilivyo makubwa ambayo UCSAF imeshayafanya na inayoendelea kuyafanya, baada ya kumsikiliza kwa makini Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Justina Mashiba, akiwasilisha utendaji wa Mfuko huo, katika Kikao kazi baina ya Mfuko na Wahariri na Waandishi wa Habari ambacho nilihudhuria kwa nafasi yangu ya Mtendaji Mkuu wa Blog ya Taifa ya CCM.
Kikao kazi hicho, kilicholenga kuujengea umma uelewa mpana juu ya utendaji wa Mfuko huo kupitia Wahariri, kiliratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), na kufanyika jijini Dar es Salaam, OTR ikiwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Umma Thobias Makoba na Afisa Habari na Mwasiliano ya Umma Mwandamizi Sabato Kosuri.
Hakika nikiri tu kwamba maelezo ya Afisa Mtendaji Mkuu Justina yalinikosha, ikiwemo aliposema kwamba UCSAF inajipanga kuwakopesha simu wananchi 'wanyonge' wa Vijijini ili kuhakikisha wanakuwa na mawasiliano ya uhakika.....
Kwa kuwa nahofia kutia au kupunguza chumvi au sukari katika mazuri aliyosema Afisa Mtendaji Mkuu huyo, nakuomba baada ya kuona picha na 'Captions' basi jitahidi usome wasilisho lake lote aliloliwasilisha kwenye kikao kazi hicho.
WASILISHO LA UCSAF HILI👇










No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇