Na Lydia Lugakila, Bukoba.
Chama cha kuweka na kukopa cha Bukoba Women Employment Association (BUWEA) katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kimebaini chanzo cha akina mama wengi kushindwa kurejesha mikopo na riba kwa wakati kuwa ni kutokana na kuwa mikopo mingi inayotokana na kuwa a utitiri wa vyama au vikundi vingi vya mikopo wanavyojitwika bila malengo.
Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya wanachama hao katika mkutano Mkuu wa Buwea Saccos uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Karumco katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba uliolenga kujadili maendeleo ya chama na kutafuta suluhu kwa baadhi ya Wanachama wanaoshindwa kutorejesha mikopo na kuona nini kifanyike ili kukomesha tatizo hilo.
Akizungumzia hali hiyo Bi Adventina Byera Mwenyekiti wa tawi la Bujugo kutoka Buwea Saccos alisema akina mama wamekuwa wakikumbana na matatizo ya kifamilia na kuwafanya kutoroka na mikopo huku baadhi yao ukopa mikopo mingi kila sehemu pamoja na kuwa na mazoea kwa vikundi hivyo.
Naye Bi Grace Mushongi alisema ni bora wadaiwa sugu kutopewa mkopo kwani wanatokomea kusiko julikana na kuacha hasara katika kundi au chama.
Kwa upande wake Wilhelemina Katera wa Ruhanga Wilayani Muleba aliomba uongozi wa Buwea kufanya ufuatiliaji na kukagua maendeleo ya vikundi mara kwa mara ili kukwepa madeni sugu huku akiwaomba akina mama kupunguza mikopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Buwea Saccos Bi Regina Majaliwa akitoa ufafanuzi zaidi juu ya uchukuaji na urejeshwaji mikopo alisema kuwa baadhi ya akina Mama kumefanya kukwamisha maendeleo ya chama kwani akina Mama ujiingiza katika mikopo mingi na mikubwa na kusahau walikoanzia.
"Hiki kikundi ni kwa ajili ya kuwakwamua Wanawake kiuchumi lakini malengo hayo yanakwenda kinyume na matarajio kutokana na mkwamo kwa baadhi ya wenzetu nashindwa kupata usingizi" alisema Bi Majaliwa.
Bi Majaliwa aliwaomba akina Mama kuweka juhudi katika kulipa kidogo kidogo, kupunguza utitiri wa mikopo waliyonayo ili wasikwamishe malengo husika.
Naye katibu wa mkutano Mkuu Buwea Saccos mwaka 2023 Odetha Alexander alisema hatua kali za kisheria zizidi kuchukuliwa kwa Mwanachama au Mwanakikundi anayechangia kudidimiza chama.
Katika majadiliano hayo kwa pamoja wanachama hao wameweka mapendekezo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchangia au kuongeza hisa, kila Mwanachama aliyechukua mkopo ahakikishe anarejesha na kumaliza ndani ya muda uliopangwa.
Hata hivyo kwa upande wake Mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Afisa ushirika Manispaa ya Bukoba Obadia Kyakajumba alisema wanachama hao wasiorejesha wanakuwa na lengo la kuua chama na kuwa uimara chama ni kukiwekea uwezo kimtaji, kuona namna ya kuongeza mapato ili kuepuka hasara.
Ikumbukwe kuwa Buwea Saccos ilianzishwa mwaka 2007 na ina Wanachama 420 kati ya hao Wanachama hai ni 403 na wasio hai ni 17 na 9 walifariki.



No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇