Na Lydia Lugakila, Bukoba.
MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imenyesha na kuleta madhara makubwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera huku ikisababisha kifo cha mtu mmoja na nyumba zaidi ya 100 zimeezuliwa na upepo huo.
Maafa hayo yametokea Oktoba 18,2023 saa 11 alfajiri, huku kata kadhaa ikiwemo Kashai, Rwamishenye na Hamugembe zikikumbwa na maafa hayo.
Akizungumzia maafa hayo Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema mtu mmoja ambaye amepoteza maisha hajafahamika majina yake na mwili wake ulionekana kuwa ulikuwa umesombwa na maji na ulikuwa haujatambuliwa.
"Maafa haya ni makubwa yamesababisha kifo cha mtu mmoja ambaye mwili wake ulipokutwa ni umesombwa na maji na katika paji la uso wake alikuwa na jeraha kama alipigwa na mti au kitu, Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi juu ya kifo hicho" alisema Erasto.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba ameongeza kuwa miongoni mwa nyumba zaidi ya 100 zilizokumbwa na maafa hayo zimo taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na Shule na kituo cha Afya pamoja na Kanisa na nguzo za umeme pamoja na miti ambavyo vimeathirika.
Aidha amewataka Wananchi Mkoani Kagera kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ili kuepukana na madhara.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Rwamishenyi Sued Kagasheki amesema kuwa alishuhudia hali hiyo akiwa anajiandaa kwenda mazoezini asubuhi ambapo alipotoka nje na kuona mvua kubwa inataka kuanza kunyesha alirudi ndani na muda mfupi mvua ilianza kunyesha ulipopita muda mfupi kama dakika 20 alianza kupokea simu kutoka kwa Wananchi wakimweleza juu ya majanga yaliyotokea.
Ametaja mitaa iliyoathirika kuwa ni mitatu kati ya minne ambayo ni Kamizilente, National housing na Rwamishenye zote za Manispaa ya Bukoba.
Aidha mmoja wa mashuhuda Padre Egidius Rweyemamu wa Parokia Rwamishenyi kanisa katoliki amesema kuwa majira ya asubuhi akiwa kanisani anasali alishuhudia kanisa la Rwamishenyi likiezuliwa na upepo na waaumini watatu wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇