LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 4, 2023

DK HAPPINES RUTA WA HOSPITALI TUMBI AZUNGUMZIA UMUHIMU WA CHAKULA BORA

 MTAALAM wa masuala ya afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Mkoani Pwani, Dk Happines Ruta amewaasa Watanzania kuzingatia chakula bora akisema hilo litasaidia kuimarisha afya na pia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Dk Happiness Ruta wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi iliyoko Mkoani Pwani


Akizungumza kwenye ziara ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwl Mwajuma Nyamka katika kata ya Kongowe, mtaalam huyo wa afya alifafanua kuwa chakula bora ni mlo unaojumuisha uwiano unaotakiwa wa virutubisho vyote muhimu vinavyotakiwa kutoka katika makundi makubwa ya vyakula.

 

Anasema kuwa miili yetu huhitaji virutubisho muhimu ili kuendelea kuwa na afya na kujilinda na magonjwa. Kuna baadhi ya virutubisho vinaweza kutengenezwa mwilini, lakini vingine lazima vipatikane kutoka kwenye chakula.

 


Kulingana na mtaalam huyo, miili ya wanadamu inapata nguvu kutoka kwenye makundi matatu ya vyakula ambavyo ni vya wanga, protini na mafuta, bila kusahau kunywa maji. Kwamba, tunahitaji vyakula hivi ili kuweza kuupa mwili nguvu na kuendelea kufanya kazi.

 

Baadhi ya vyakula vilivyo na wanga ni : viazi, vyakula vya nafaka (mchele, mahindi, mtama) na vinginevyo. Aidha vyakula vyenye protini ni kama samaki, nyama, maharage na mayai. Vyakula vyenye  madini na vitamini kwa wingi ni matunda na mboga za majani.

 

Unashauriwa kutumia zaidi mafuta yatokanayo na mimea na viumbe wa baharini tofauti na yale yanayotokana na wanyama na viwandani. Mafuta ya samaki huwa na omega fatty acids ambazo ni muhimu katika kukuza ubongo. Mafuta mabaya huufanya mwili ushindwe kushamiri na hivyo kupata matatizo zaidi.

 

Mtaalam huyo anasema ili Taifa liendelee kuwa imara ni muhimu sana kwa wananchi kula vyakula bora, akisema kuwa vyakula hivyo vinapatikana kabisa katika maeneo yetu tunayoishi.

 

“Vyakula bora tunavyo majumbani mwetu, ni suala la kuvitumia tu, naomba sana Watanzania wenzangu tusile tu ili mradi tumbo limejaa, tuzingatia vyakula bora,” anasisitiza Dk Ruta.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages