NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
WAAJIRI wamesema pesa wanayochangia kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) haipotei bure kwani ni kwa maslahi ya pande tatu, Mwajiri, Mfanyakazi na Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofikia kilele leo Julai 13, 2023 wameishukuru Serikali kwa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwani unatoa hakikisho la usalama wa Mfanyakazi.
“Tayari tumeanza kuchangia, tuchukue nafasi ya kuelimishana ndani kwamba iko fursa ndani ya WCF kuwahudumia wafanyakazi pindi wanapokumbwa na madhila wawapo kazini.” Alisema Akbarali ambaye ni mwajiri kutoka kampuni yakutengeneza magari makubwa ya GF iliyoko Kibaha.
Kiwanda cha GF kina miaka mitatu tangu kianze kufanya kazi na kina jumla ya wafanyakazi zaidi ya 300 ambao wanachangiwa kwenye Mfuko wa WCF.
Bw. Akbarali alisema, alifika kwenye banda la WCF ili aweze kupata uelewa zaidi kuhusu huduma zitolewazo na WCF ingawa kampuni yake tayari ilijisajili kama takwa la kisheria.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambaye naye ni mwajiri Bw. Elihuruma Mabelya amesema Manispaa ya Temeke inao wafanyakazi zaidi ya 5,600 lakini pia ina idadi kubwa ya viwanda vikiwemo vikubwa na vidogo hali inayofanya WCF kuwa mdau muhimu wa Manispaa hiyo.
“WCF kwetu kama Temeke imekuwa kama mkombozi, kwasababu wafanyakazi wanapopatwa na ajali au matatizo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao Mfuko unakuja kusaidia na hivyo kutoathiri uzalishaji mali unaoendelea ndani ya Wilaya yetu,” alisema.
Aliipongeza WCF kutokana na kuchukua jukumu la kumuinua mwananchi ambaye ni Mfanyakazi na mwsiho wa siku kuinua uchumi wa Halmashauri na kuinua uchumi wa Taifa.
Naye Bw. Dofrian Junwalji kutoka Taasisi ya Trias Tanzania inayowawezesha Wajasiriamali alisema elimu aliyoipata kwenye banda la WCF imemuwezesha kupata uelewa zaidi na ametambua umuhimu wa WCF kiuchumi kwa mwajiri na mwajiriwa.
“Mfanyakazi anapoumia maana yake atakuwa hazalishi, kwahivyo WCF ina beba jukumu la kumuwezesha kujikimu kimaisha kwa kumlipa fidia kwa hivyo mzunguko wa fedha unakuwepo, ataendelea kupata mahitaji yake kama vile chakula, kulipia pango na mahitaji mengine.” Alifafanua Bw. Junwalji.
Alitaja manufaa mengine kuwa ni pale Mwajiriwa anapokumbwa na matatizo ya kuumia au kuugua WCF inamuhudumia na hivyo mwajiri anabaki akiendelea na shughuli zake za uzalishaji na ikibidi Mfuko unamfidia gharama alizoinhia mwajiri kumuhudumia manyakazi wake.
‘Ningependa kuwashauri waajiri kujisajili na Mfuko kwani kwakufanya hivyo matokeo ya uamuzi wa kufanya hivyo yatakuja kuonekaan baadaye na uchangiaji wenyewe ni asilimia 0.5 tu ya mshahara wa mwajiriwa.” Alihitimisha.
Akitoa tathmini yake mara baada ya kutemebela banda la WCF na kujionea jinsi waajiri na wafanyakazi wanavyopatiwa huduma, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi alisema, WCF inafanya kazi nzuri licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanzishwa kwake.
“Nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu Dkt. Mduma pamoja na Bodi ya Wadhamini, wanafanya kazi kubwa na nzuri na ya mfano kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.” Alisema.
Katika eneo la utoaji huduma, alisema zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote za WCF zinatolewa kwa njia ya TEHAMA.
“WCF ina watu wenye weledi wa kutosha lakini niwahakikishie waajiri na wafanyakazi kuwa ustahimilivu wa Mfuko huu ni wa uhakika hata kama itatokea 2050 Mfuko haujafanya chochote unao uwezo wa kuwahudumia wateja wake.” Alitoa hakikisho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amewahakikishia waajiri na wafanyakazi kuwa Mfuko uko imara katika kuhakikisha unatekeleza wajibu wake wa kulipa fidia stahiki na kwa wakati endapo mfanyaklazi ataumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
“Tunayafanya haya ili kuhakikisha kwamba wawekezaji waliopo sasa na wanaokuja wakute nguvu kazi ya Tanzania ikiwa salama, na wale watakaopatwa na madhara yatokanayo na kazi Mfuko wa WCF utatumika kuwalipa fidia zao stahiki, kuwalipia matibabu yao ili kuhakikisha wanarejea kazini haraka iwezekanavyo.” Alitoa hakikisho.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akimpatia maelezo ya masuala yahusuyo fidia kwa wafanyakazi, mwananchi huyu aliyetembelea banda la WCF.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila (mwenye balaghashia) akishukuru baada ya yeye na ujumbe wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi (wapili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke Bw. Elihuruma Mabelya, walipopewa elimu kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (kulia).
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akifafanua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na WCF kwa baadhi ya waajiri hawa waliotembelea banda la Mfuko huo.
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi WCF, Bi. Veronica Saeni (kushoto) akimuhudumia mwananchi aliyetembekea banda la Mfuko huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu (wanne kulia), Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma (watano kulia) na baadhi ya wafanyakazi wa WCF.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇