NA HEMEDI MUNGA
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewataka wafanyabiashara mbalimbali wilayani hapa kufuatilia fursa ya mikopo itolewayo na Benki ya NMB.
Mwenda ametoa wito huo wakati akizungumza na wafanyabiashara hao katika semina ya kuwaelimisha kuhusu utaratibu wa uuzaji, ununuzi na urasimishaji wa biashara ya mazao ya kilimo hapa nchini.
Alisema kunafursa za mikopo ambazo huwanufaisha watu si tu Tanzania hata nchi zilizoendelea hukopa huku nyingine zikiendesha uchumi wake kwa kutegemea sekta binafsi kwa zaidi ya asilimia 90.
"Ndugu zangu msiogope kwenda kukopa kwa sababu hakuna mfanyabiashara sio Iramba tu duniani hakopi," alisisitiza.
Alisema ukiwa mfanyabiashara ni lazima uwe mtu wa kuchukua uthubutu au hatari (risk) na hiyo ndio maana ya biashara, hivyo msiogope kwa sababu taasisi hizo zipo kwa ajili ya kuwasaidia.
"Kopeni mkafanye biashara hakuna duniani mfanyabiashara anayeendelea na kutajirika bila mkopo hayupo," alisisitiza.
Aidha, alifafanua kuwa sio mfanyabiashara tu hata nchi hakuna inayoendelea bila yakuwa na mikopo huku akitolea mfano wa nchi kubwa na zenye uchumi mkubwa ikiwemo Marekani, China na Ujeruman.
Aliwataka wakakope kwa lengo la kununua mazao na kuyapeleka sokoni.
Kwa upande wa Meneja wa Benki hiyo tawi la Kiomboi, Juma Sololoka aliwataka wafanyabiashara hao kuzingatia masharti au kukizi vigezo mbalimbali yatakayowawezesha kunufaika na mikipo hiyo.
Alisema wanamsaidia mkulima, watu wa mazao, pembejeo, wasindikaji na wauzaji wa vyakula.
Aidha, aliipongeza Benki hiyo, imetenga takribani sh bilioni 200 ambapo wanakopesha kuanzia sh milioni moja hadi bilioni moja kwa mfanyabiashara mdogo huku riba yake ikiwa ni asilimia tisa tu.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo wilayani hapa, Marietha Kasongo alisema Wizara ya Kilimo imeweka utaratibu huo kwa lengo la kuimarisha biashara ya mazao nchini.
Alisema serikali inampango wa kuwalinda wakulima na wafanyabiashara dhidi ya usumbufu na utapeli unaotokea katika biashara ya mazao ya kilimo.
Aidha, kuimarisha sekta ya Kilimo Mazao kwa lengo la kuwezesha ufanyaji wa biashara kwa mujibu wa sheria na taratibu, kuwalinda wafanyabiashara wa ndani dhidi ya wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania wanaonunua mazao moja kwa moja shambani.
Pia, kuwasaidia wakulima wa Tanzania kunufaika kutokana na jitihada za serikali za kutoa ruzuku na uwekezaji unaoendelea kwa lengo la kupunguza gharama za kilimo na kuongeza uzalishaji na kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za biashara ya mazao ya kilimo.
Wafanyabiashara wakisikiliza maelekezo ya Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda wakati akizungumza nao katika semina ya kuwaelimisha kuhusu utaratibu wa uuzaji, ununuzi na urasimishaji wa biashara ya mazao ya kilimo hapa nchini, leo. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa wilaya)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇