Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25, Julai. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa ameongoza viongozi na wananchi katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kikosi cha 21 JWTZ Kaboya, Wilaya ya Muleba.
Akizungumza na wananchi mara baada kuwaombea Dua/Sala na kutembelea makaburi ya mashujaa hao waliopigana vita vya Kagera mwaka 1978-1979, amewataka wananchi kuendelea kuwaenzi mashujaa hao kwa vitendo kwa kulinda rasilimali za Nchi yetu na kuwa wazalendo kama mashujaa hao waliojitoa kwa ajili ya Nchi yetu.
“Leo tumekutana katika viwanja hivi kuwakumbuka na kuwaombea ndugu zetu waliopoteza maisha yao wakati wakitetea, wakipigania na kuulinda uhuru wa Nchi yetu. Tunao mashujaa wengi walioshiriki katika harakati mbalimbali za kupigania Uhuru na kulinda Taifa letu la Tanzania. Baadhi yao ni hawa waliolala hapa Kaboya lakini wapo wengine wengi katika maeneo mengine wakiwemo waliopumzika pale Songea,” ameeleza Mhe. Mwassa
Ameendelea kueleza kuwa tunapoikumbuka historia tunatambua kwamba wapo wa Tanzania waliotoa maisha yao kwa nyakati mbalimbali kupambana na utawala dhalimu wa Kijerumani kama vile Mtemi Mirambo wa Tabora, Mangi Meli wa Kilimanjaro na Mtemi Mkwawa wa Iringa katika miaka ya 1890. Wapo pia ndugu zetu waliopoteza maisha wakati wa majimaji chini ya hamasa ya Kinjekitile Ngwale kati ya mwaka 1905 na mwaka 1907.
Akimnukuu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliposema “Heshima ya mtu itokane na huduma yake kwa Umma” ameeleza kuwa wapo watu wanadhamana kubwa lakini hawazitumii vizuri, hivyo kupitia maadhimisho hayo amewakumbusha Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wote wanaohatarisha Uhuru na usalama wa Nchi yete
Hawa ni pamoja na wale wanaoshiriki kuwaandikisha na kuwapa nyaraka mbalimbali za uraia watu ambao si Watanzania.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa katika Maadhimisho hayo,Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Dkt. Abel Nyamuhanga amewasihi Watanzania kuendelea kuwaombea Dua/Sala watu wote waliopoteza uhai wao wakati wakipambania Nchi yetu.
Jumla ya Mashujaa 619 waliopigana katika vita ya Kagera dhidi ya Idd Amin Dada mnamo mwaka 1978 hadi mwaka 1979, walizikwa katika eneo la kikosi cha 21 JWTZ kambi ya Kaboya, Wilaya ya Muleba.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇