Na Oscar Assenga,Tanga
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tanga Alhaj Hasani Ramadhani Mbezi ameshauri na kuelekeza Jumuiya za Wazazi za wilaya za mkoa huo kuhakikisha zinakuwa na maono ya maendeleo na kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali.
Alhaj Mbezi alisema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wazazi la Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga kilichoketi kupokea Taarifa ya kazi kwa kipindi cha miezi Sita kuanzia Januari mpaka June 2023.
Alisema kwa sababu haiwezekani Jumuiya kuwa ombaomba wakati wanaweza kubuni na kuweka mikakati ya kuanzisha vitega uchumi ambavyo vinaweza kuwa chachu ya kujikwamua kiuchumi.
“Kwa kweli haiwezekani Jumuiya kubwa kama Wazazi kuwa ombaomba wakati tunaweza kufanya mambo yakatusaidia kiunuka kiuchumi hivyo niagize tuanzisheni miradi ya kiuchumi kwani Tanga kuna ardhi kubwa na miradi mingi hasa kilimo cha Mkonge lakini kubuni na kuanzisha Sheli mbalimbali”Alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha alisema pia Jumuiya hizo zinaweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa mfano vya kufyetua matofali ambayo vitawasaidia sana wazazi Tanga mjini.
Umoja na mshikamano
Alhaj Mbezi alisema umoja na mshikamano ndio mafanikio makubwa katika jambo lolote hivyo wanapaswa kuuimarisha na kusimama kidete ili uchaguzi 2024/2025 kuhakikisha wanachukuia viti vyote kuanzia ngazi ya chini mpaka udiwani.
Alisema watakapofanya hivyo itawapa dira ya kuelekea 2025 kuhakikisha kura zote za mkoa wa Tanga zinakwenda kwa Rais Dkt Samia Suluhu ambaye ni msikivu mpenda watu.
“Kwa mkoa wa Tanga ametupendelea leo tunajenga daraja mto Pangani ambalo ni kubwa tokea uhuru tuna kila sababu ya kusema Tanga tunakuwa wa kwanza kwa kura za Rais Dkt Samia”Alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilaya ya Tanga Hamza Bwanga alisema Jumuiya hiyo ipo tayari kuonyesha nguvu yake kwa kutoa mchango wake mkubwa kwenda kushirikiana na viongozi mbalimbali na wananchi kuhakikisha 2024 wanachukua viti vyote katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Nikuhakikishie Mwenyekiti sisi Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Tanga tutakuwa mstari wa mbele kupigana usiku na mchana kuwa tayari kukitumikia chama na kuonyesha mchango wetu kuhakikisha kinapiga hatua kubwa za kimaendeleo”Alisema Mwenyekiti Hamza.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe wa mkutano huo ukimalizika wahakikishe wanaporudi kwenye kata zao kuhakikisha mabaraza yanafanyika kikatiba,wanaelimisha pamoja na mabaraza ya matawi.
Hata hivyo alisema wahakikishe pia wanaunda kamati ndogo za mazingira elimu na uchumi ili waweze kuwasaidia kuhakikisha jumuiya ya wazazi inakuwa imara na kushika namba moja mkoa huo na itakuwa na mchango mkubwa kwenye Chama cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇