Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Daniel Chongolo amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuilinda amani, amesema kuwa hiyo ni mojawapo ya tunu ambazo waasisi wa Tanzania walihakikisha inakuwa ni utambulisho wa taifa na inatakiwa kulindwa na kutetewa kwa nguvu zote bila kuwaonea aibu wala kuwaogopa wote wanaotishia kuivuruga kwa maslahi ya kisiasa.
“Mwalimu (Nyerere, Baba wa Taifa) alisema ukiulizwa Tanzania una nini, sema una amani huku ukijidai. Amani hii si amani rahisi, si amani ya lelemama, kuna watu wametoka jasho na wanatoa jasho ili hii amani iwepo. Tusiache amani hii ipotee kwa sababu ya wajanja wachache wenye dhamira ovu kwa nchi yetu, wenzetu wana mahali pa kukimbilia.”
“Na ushahidi tumeuona miaka michache iliyopita. Walivyoona huku mambo yao yamekaa vibaya walitafuta pa kuishi. Sisi tuna wapi pa kukimbilia nje ya Tanzania? Kama hatuna tujue tuna wajibu wa kuilinda amani ya nchi hii, tuna wajibu wa kuiendeleza nchi hii. Na tuna wajibu wa kusimamia maslahi ya nchi hii bila aibu wala kumuogopa yeyote,” amesema Ndugu Chongolo akisisitiza pia kuwa CCM itahakikisha maoni ya wananchi yenye tija na chanya, yanafanyiwa kazi na Serikali katika hatua za kuingia mkataba wa utekelezaji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇