LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 2, 2023

WAZIRI WA AFYA UMMY MWALIMU ATANGAZA RASMI KUISHA MARBURG KAGERA.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika Tukio la kumalizika mlipuko wa Ugonjwa wa Marburg Kagera.


Na Lydia Lugakila, Bukoba.


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetangaza rasmi kuisha ugonjwa wa Marburg ambao ulisababisha vifo sita kutoka katika kata za Matuku na Kanyangereko Mkoani Kagera.


Hali hii imekuja baada ya wataalam wa afya hapa nchini kwa kushirikiana na shirika la afya ulimwenguni (WHO) kuthibitisha kuwa mlipuko huo haupo tena eneo katika eneo hilo.


Akizungumza katika Tukio la kutangaza kumalizika kwa mlipuko wa Ugonjwa Marburg limefanyika katika ofisi za Mkoa wa Kagera, Waziri wa Afya, Ummy  Mwalimu alitoa shukrani za pekee kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Viongozi wengine wa Afya hapa nchini, Serikali za Umoja wa Ulaya, Serikali ya Marekani na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na kutangaza kuwa ugonjwa huo mlipuko huo umeisha rasmi katika Mkoa huo.


"Tanzania ipo salama kwa umoja wetu nguvu zetu na ushirikiano wa pamoja tumeweza kuuthibiti ugonjwa huo" alisema Waziri Ummy.


Aidha Waziri Ummy kupitia Serikali ametoa Shilingi Milioni tano kwa ajili ya familia ya Mtaalam wa Maabara katika Kituo cha Afya Maruku aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa huo huku akieleza kuwa Serikali tayari imeweka mkakati wa kutumia shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa vituo maalum vya afya katika maeneo ya mipakani kwa ajili ya uimarishaji na ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu, akitoa taarifa fupi juu ya mwenendo wa Ugonjwa huo  alisema mnamo Machi 16 mwaka huu, ugonjwa huo uliibuka katika Kata za Maruku na Kanyangereko zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera na mgonjwa wa mwisho alipona aprili 19 mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo na baada ya siku 42 tangu kutokea kwa tukio hilo kwa sasa Tanzania ipo salama kwa mujibu wa sheria za afya ulimwenguni.


Naye Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila ameanza kwa kumshukuru Rais Samia  na Waziri huyo wa Afya kwa ushupavu wao katika utendaji kazi kwa kuyapigania Watanzania na kuiomba Wizara ya Afya kujenga Hospitali maalum ya kuhudumia wagonjwa wa magonjwa hatari ya mlipuko, Kituo maalum cha kuratibu magonjwa hayo, kuwapo kwa idara ya afya katika mipaka ya Mkoa huo na nchi jirani, Upanuzi wa Hospitali ya Rufaa na chuo cha Afya Kagemu, Wataalam 48 wa magonjwa ya mlipuko kuendelea kujengewa uwezo wa kitaaluma.


Hata hivyo tukio hilo limewakutanisha  pamoja Viongozi mbalimbali wakiwemo, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wawakilishi wa Wizara na taasisi mbalimbali, madiwani, vyombo vya ulinzi na usalama na madaktari  mbali mbali wa ndani na nje ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages