Na K-Vis Blog/Khalfan Said
MBUNGE
wa Jimbo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Mhe. Abdallah Chaurembo
amewaambia wapiga kura wake wa Mbagala Kiburugwa kujiandaa na zoezi la
urasimishaji ardhi/majengo linalotarajiwa kuanza hivi karibuni kwenye
eneo hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na
uongozi wa Serikali ya mtaa wa Kiburugwa kwenye viwanja vya Kwa-Njau,
Juni 4, 2023, Mhe. Chaurembo alisema urasimishaji wa ardhi/majengo ni
kutambua miliki za wananchi kwenye maeneo yaliyoendelezwa bila kupimwa
kisheria.
“Wengi wenu mnamiliki ardhi au nyumba kwa kutumia
makaratasi mliyoandikishiana ambayo hayatambuliki kisheria na baadhi
yenu mna leseni za makazi ambazo zilikuwa za kipindi cha muda fulani na
nyingi zimekwisha muda wake na matokeo ya urasimishaji ni kutoa
hatimiliki inayotambulika kisheria.” Alifafanua.
Alisema zoezi
hilo ni shirikishi na kwamba wananchi wakiafiki, wataletwa wataalamu wa
upimaji ardhi na kutoa elimu ya jinsi zoezi hilo litakavyoendeshwa ikiwa
ni pamoja na gharama ambazo mwananchi anapaswa kuchangia ili
ardhi/jengo lake liweze kupimwa na kupatiwa hati miliki ya serikali.
Alisema
urasimishaji mbali na kuipa thamani ardhi/nyumba lakini pia utasaidia
kuboresha makazi hususan kwa kuweka miundombinu ya msingi ili
kurahisisha usafiri, kupunguza madhara yatokanayo na majanga mbalimbali
kama vile mafuriko na moto.
Zoezi la urasimishaji lilizinduliwa
mwaka 2013 na aliyekuwa waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makzi,
Mhe. William Lukuvi na limefanyika maeneo mbalimbali ya nchi na lengo
lilikuwa ifikapo mwaka huu wa 2023 liwe limekamilika.
Awali
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kiburugwa Bw. Abdallah Mpili pamoja na
kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu mtaa huo ikiwemo masuala ya
ulinzi jamii, usafi wa mazingira, ujenzi wa ofisi ya Srrikali ya mtaa,
aliwahakikishia wananchi kuwa zoezi hilo litafanyika kwa uwazi na kwa
kushirikisha wananchi.
“Wapima
ardhi watakapokuja hapa tutajadiliana nao na kukubaliana jinsi zoezi
litakavyoendeshwa ikiwa ni pamoja na gharama ambazo kila mwananchi
(mwenye ardhi.nyumba) atapaswa kuchangia." Alisema Mpili
MBUNGE wa Jimbo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Mhe. Abdallah Chaurembo akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kiburugwa Juni 4, 2023
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇