Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo ameshangazwa na jengo kukaa zaidi ya miaka kumi bila kukamilika na Serikali ilishaleta fedha za kuanzisha ujenzi wake.
Katibu Mkuu ameyasema hayo mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika kata ya Msaada, wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
“Ndugu zangu niseme mimi nimeshangazwa kidogo na jengo kukaa miaka 13 bila kumaliziwa na serikali ilishaleta fedha za kuanzisha ujenzi wake, maeneo ya Utawala yanapogawanywa hayatakiwi kuwa kikwazo cha mambo kuendelea, lazima yawe ni urahisishaji wa usogezaji huduma kwa wananchi” alisema Katibu Mkuu.
Chongolo ameahidi kusukuma fedha shilingi milioni 150 za kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la Mama na Mtoto kwa sababu afya ni muhimu sana haswa afya ya mama na mtoto wakati wa kujifungua na kabla ya kujifungua.
Katibu Mkuu yupo kwenye ziara mkoani Dodoma ya kukagua,kuhamasisha na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025, ambapo leo alikuwa katika wilaya ya Chemba akiwa ameongozana na Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇