LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 24, 2023

RAIS DK. MWINYI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WAZIRI WA MAMBO YA NISHATI QATAR, LEO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya Qatar akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Dk. Samia Suluhu Hassan, mapema leo asubuhi alikutana na Waziri anayeshughulikia masuala ya Nishati wa Qatar Mhe. Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi.


Katika mazungumzo hayo walijadili juu ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Qatar kuhusiana na uchimbaji wa mafuta na gesi Zanzibar. Mkutano huo ulilenga namna ambavyo nchi hizo mbili zinaweza kufanya kazi pamoja katika eneo hilo.


Dk. Mwinyi alimfahamisha Waziri huyo wa Qatar kuhusu sera ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu na jinsi Qatar inaweza kuwa msaada katika suala la uchimbaji wa rasilimali hiyo. 


Dk. Mwinyi amemwambia Waziri wa Nishati wa Qatar kutuma wataalamu wake Zanzibar ili kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa Zanzibar kuchunguza uwezekano wa kuanza haraka uchimbaji wa rasilimali hizi. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja na ujuzi wa kitaalam kutoka Qatar unaweza kuchochea maendeleo na utekelezaji wa uchimbaji huo kwa ufanisi na kwa kasi.


Waziri wa Nishati wa Qatar, Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi, alimjibu Mhe. Dk. Mwinyi akielezea kuwa nchi yake tayari ina uzoefu wa kufanya kazi na mataifa ya Afrika katika uchimbaji wa mafuta na gesi. Alikuwa wazi kuwa Qatar imekuwa ikisaidia nchi nyingi barani Afrika katika sekta hii na iko tayari kuendelea kufanya hivyo na Zanzibar.


Baadae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikutana na Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Mh. Jassin bin Saif Ahmed. Katika mkutano huo, Dk. Mwinyi alimuelezea Waziri wa Uchukuzi wa Qatar kuhusu mipango ya Zanzibar kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, ambayo itakuwa kituo kikuu cha kupakia na kupakua mizigo. Dk. Mwinyi alipendekeza kuwa Serikali ya Qatar inaweza kutoa msaada katika ujenzi wa bandari hiyo.


Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Mhe. Jassin bin Saif Ahmed, alionyesha shauku kubwa kuhusu mradi huo, hasa baada ya kupewa taarifa kuwa eneo la ujenzi wa Bandari ya Mangapwani lina kina cha mita 18, ambacho ni kina kinachofaa kwa meli kubwa za mizigo. Hii inaashiria uwezekano wa Qatar kuwa sehemu ya ujenzi na maendeleo ya bandari hiyo.

Tazama Video hapo👇


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages