KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusimamia vizuri ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi iliyopo katika Kata ya Mboliboli katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ili ikamilike kwa wakati.
Skimu hiyo inajengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Sh. Bilioni 58 na inatarajiwa kutumika kwenye mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 15,000 zilizopo kwenye eneo hilo ambalo wananchi wanazalisha mpunga.
Katibu Mkuu Chongolo alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kukagua skimu hiyo kwa lengo la kuangalia maendeleo yake ambapo aliipongeza serikali kwa kuamua kujenga skimu hiyo.
Alisema mradi huo unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 18 kama ambavyo mikataba ya wakandarasi wanaotekeleza imeainishwa ili wananchi waanze uzalishaji mapema na kuongeza tija ya kilimo katika eneo hilo.
“Naipongeza sana serikali kwa kuanzisha mradi huu lakini ili tija yake ionekane tume ya taifa ya umwagiliaji inatakiwa kusimamia vizuri, sisi huko serikalini tutaweka msukumo ili fedha za kuwalipa wakandarasi zije kwa wakati,” alisema Chongolo.
Aliwataka wananchi watakaokuwa wanaitumia skimu hiyo kuhakikisha wanaitunza miundombinu ili itumike kwa muda mrefu na tija yake iendane na fedha ambazo serikali imewekeza katika eneo hilo.
Ofisa Umwagiliaji wa Wilaya ya Iringa, Mhandisi Julius Lazaro alisema skimu hiyo ilianzishwa na wananchi ambao walikuwa wanaitengeneza kwa kutumia mbinu za kienyeji na hivyo tija yake ilikuwa ndogo kwa sababu walikuwa wanazuia maji na mchanga.
Alisema wananchi hao walikuwa wanalima ekari 5,000 pekee kwa mwaka mzima lakini watakapokamilisha ujenzi wa skimu hiyo watakuwa wanalima zaidi ya ekari 15,000 ambazo zipo kwenye bonde hilo.
Alisema uzalishaji wa sasa ni tani 6,000 za mpunga lakini skimu hiyo itakapoanza kutumika uzalishaji utaongezemka mara sit ana kufikia tani 36,000 na hivyo kuwainua wananchi wa eneo hilo kukua kiuchumi.
“Mkataba wa ujenzi wa skimu hii ni wa miezi 18 na ikikamilika itawasaidia wakulima kulima mara mbili kwa mwaka tofauti na sasa ambapo wanalima mara moja pekee,” alisema Mhandisi Lazaro.
Diwani wa Kata hiyo ya Mboliboli, Yusuph Samba aliishukuru serikali kwa kuwasaidia kuboresha skimu hiyo kwa maelezo kuwa walikuwa wanapata shida kwa muda mrefu na kulikuwa kunaibuka migogoro mingi.
Alisema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakijituma kwenye shughuli za kilimo lakini tatizo lililokuwa likiwakabili ni ubovu wa miundombinu ya umwagiliaji.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema aliwataka wananchi hao kutouza chakula chote baada ya kuvuna kwa maelezo kuwa wanaweza wakakumbwa na tatizo la njaa na hivyo kusababisha uudumavu kwa watoto.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇