Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo amesema msimamo wa CCM ni nchi kuwa na mitaala itakayotoa elimu ya taaluma za kukitegemea kimaisha kuliko ya kutegemea kuajiriwa.
Chongolo ametoa msimamo huo Mei 28, katika Mkutano wa hadhara katika kata ya Malangali wilayani Mufindi mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 7 ya kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa ruhusa kwa kamati na inaendelea kupitia mitaala hiyo itakayokidhi soko pamoja na kupata vijana watakaoanza kusoma taaluma ambayo inaweza kumsaidia kujiajiri.
Katika hatua nyingine Chongolo amesema Serikali imetatua changamoto ya pembejeo ikiwemo mbolea ambapo kwa sasa Serikali imeweka ruzuku na hivyo kufanya bei kushuka na hivyo wakulima wengi kumudu kununua.
Amesema Serikali inaendelea kushughulikia upatikanaji wa haraka na urahisi kwa wakulima hivyo amewataka kuendelea na kilimo kwa kuwa tatizo hilo linaendelea kushughulikiwa.
Aidha Chongolo amesema Serikali inafanya kazi kubwa kwa kuwa inajua dhamira na wajibu wake ni kutoa huduma kwa wananchi hivyo wataendelea kusimamia ili huduma muhimu ziwafikie wananchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇