DC MWENDA AMPONGEZA RAIS DK. SAMIA SULUHU HASSAN
Na HEMEDI MUNGA
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida, Suleiman Mwenda ameendelea kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotoa takribani sh bilioni 1.4 katika kata ya Urughu kati ya kata 20 za wilaya hiyo.
Anasema huo ni upendo mkubwa sana wa Rais Dk. Samia kuwajali wananchi wa kata hiyo, hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kumuombea na kumuunga mkono Rais huyo.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mang'ole na Mlandala vilivyopo kata ya Urughu Tarafa ya Ndago wilayani hapa katika ziara yake ya kuelezea kazi zilizofanywa na Rais Dk. Samia ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani, Mwenda anasema wananchi wanakila sababu ya kumshukuru na kumuunga mkono Rais huyo.
‘’Ndugu zangu huku ni kutujali kwa kiwango cha hali ya juu yani ndani ya kata moja tu Rais Dk. Samia katupa sh bilioni 1.4 zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,’’anasema.
Aidha, anaongeza kuwa kiwango hicho cha fedha na zaidi katika kata nyingine za wilaya hiyo kipo na miradi ya maendeleo inaendelea vyema.
Halikadhalika, Mwenda anafafanua kuwa mafanikio hayo ni ya ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dk. Samia, hivyo amewataka wananchi hao kutarajia makubwa katika miaka ijayo ya uongozi wake.
Mbali na hayo, Mwenda amewahakikishia wananchi hao kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kufikisha umeme katika kila kijiji na kitongoji.
‘’Tumeanza vyema kuhakikisha vijiji 70 vya wilaya hii vinanishati ya umeme na tunaimani ifikapo 2026 vitongoji 393 vitakuwa vimepata nishati hii,’’anasema.
Pia, Mwenda anawataka wananchi hao kufahamu kuwa yapo maendeleo makubwa katika maeneo mengine ya wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la kupokelea wagonjwa wa dharura na jengo la wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).
Anafafanua kuwa Rais Dk. Samia aliteta fedha zilizowezesha kujenga miundombinu hiyo huku akifanikisha kujenga vituo vya afya saba.
Anasema mafanikio hayo ni ya kasi ya ajabu kwa sababu tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi hii wilaya hiyo ilikuwa na vituo vya afya viwili tu.
Aidha, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dk. Samia amejenga vituo vya afya saba na zahanati nyingi.
DC Mwenda yupo katika ziara ya kijiji kwa kijiji kuelezea kazi zilizofanywa na Rais Dk. Samia ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani.
Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida, Suleiman Mwenda akiwaeleza wananchi wa vijiji vya Mang'ole na Mlandala vilivyopo kata ya Urughu Tarafa ya Ndago wilayani hapa leo katika ziara yake ya kuelezea kazi zilizofanywa na Rais Dk. Samia ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani. (Picha na Ahmed Makame)
Afisa Tawala ambaye ni kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida, Linda Koka akiwataka wananchi kuwa wasikivu wa kazi za maendeleo zilizofanywa na Rais Dk. Samia ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani. (Picha na Ahmed Makame)
Wananchi wa vijiji vya Mang'ole na Mlandala vilivyopo kata ya Urughu Tarafa ya Ndago wilayani hapa wakisikiliza mafanikio aliyoyafanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani. (Picha na Ahmed Makame)
Wananchi wa vijiji vya Mang'ole na Mlandala vilivyopo kata ya Urughu Tarafa ya Ndago wilayani hapa wakisikiliza mafanikio aliyoyafanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili tangu aingie madarakani. (Picha na Ahmed Makame)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇