NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MOROGORO.
MNUFAIKA
wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Deus Anthony, ameushukuru Mfuko huo
kwa kumuwezesha kuyamudu maisha licha ya kupata Ulemavu wa Kudumu uliotokana na
Kazi.
Mnufaika
huyo mkazi wa Morogoro ameyasema hayo jana Aprili 27, 2023 kwenye Maonesho ya
Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwenye viwanja vya Tumbaku
mjini humo.
“Nilikatika
mguu wa kushoto wakati nikiwa kazini
mwaka 2017, WCF wamekuwa na mimi katika matibabu hadi kupona.”
Alisema
hawakuishia hapo, “Nilipata Ulemavu wa Kudumu, wameninunulia mguu wa bandia
naweza kutembea vizuri bila ya shida yoyote,” amefafanua.
Bw.
Deus ambaye wakati anaumia kazi yake ilikuwa ni udereva amesema pensheni ya
kila mwezi anayolipwa na WCF ameweza kudunduliza na kununua bajaji.
“Nawashukuru
WCF kwa kuniwezesha kuyamudu maisha, hivi sasa nafikiria kukodi shamba ili
nilime maaharage huko Mikumi.” Amesema
Kuhusu
ushiriki wa WCF kwenye Maonesho hayo yanayofanyika Kitaifa mjini humo,
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar amesema pamoja na kulipa fidia Mfuko unalo jukumu la kukuza mbinu za kuzuia
ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi lakini pia kutoa elimu kwa Umma;
“Na
hapa ndio mahala pake, hapa tunakutana na wananchi, tunakutana na wafanyakazi
lakini pia tunakutana na waajiri, hivyo hii ni fursa nzuri kwetu na kwa wadau
wetu pia.” Alisema Dkt. Omar.
Alisema
katika banda la WCF wanatoa Elimu ya Fidia kwa njia mbalimbali ikiwemo michoro
inayoonyesha tofauti ya viwango vya Ulemavu vinavyotumika kulipa fidia.
Aidha
Meneja Tathmini na Usalama mahali pa Kazi WCF, Bi. Naanjela Msangi amesema
katika kukuza mbinu za kuzuia ajali,
magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi wanatoa Elimu kwa nadharia lakini pia
kuna vifaa mbalimbali vya kujihami dhidi ya majanga kazini.
“Tunaonyesha
vifaa sahihi vya kujihami kama vile mask (N95) kuzuia vumbi (normal dust), mask
za kuzuia vumbi lenye kemikali, full face, Kifaa cha kupima viwango vya kelele
maeneo ya kazi, kupima viwango vya mitetemo mwili mzima na mikono, kifaa cha
kukinga kelele (ear muff), safety boots, reflectors na overall, hand
gloves." alifafanua.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi hufanyika Aprili 28 kila mwaka ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuiadhimisha siku hii, lengo kubwa ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi ambapo kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwakam huu ni “Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kushoto) akitumia mchoro kumuelimisha Mwenyekiti wa TAMICO Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM), Bw. Julius Stephen alipotembelea banda la WCF Aprili 27, 2023.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇