Benki ya NMB inaendelea kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia kampeni ya #MitiMilioni nchi nzima, na wiki jana waliadhimisha athma hio mkoani Tabora kwa ajili ya mikoa ya kanda yake ya magharibi kwa kupanda zaidi ya 3,000 katika kambi ya Magereza Kazima.
Zoezi hili la upandaji miti liliongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Rogath Mboya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Balozi Dkt. Batilda Burhan.
Pia walikuwepo watendaji wa Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Taasisi hiyo ndiyo inayoratibu zoezi zima la mradi wa NMB wa kuikijanisha Tanzania.
Ujumbe wa NMB inayoendesha kampeni hiyo kama sehemu ya ajenda yake ya uendelevu uliongozwa na Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu, Bw Emmanuel Akonaay.
Miongoni mwa vitu alivyovibainisha Bw Akonaay ni kwamba mwaka huu wameongeza TZS bilioni 2 kwenye bajeti ya kuwajibika kwa jamii (CSR) hadi TZS bilioni 6.2 kwa ajili ya kufadhili michakato ya maendeleo endelevu.
Ongezeko hilo ndilo NMB inalolitumia kufadhili kampeni ya kupanda miti milioni moja ambao ni uwekezaji uliopongezwa sana na wakazi wa Tabora.
Bw Akonaay alisema mbinu nyingine ya kuhakikisha ufanisi wa kampeni hiyo ni ushirikishwaji wa wanafunzi kupitia shindano la upandaji miti mashuleni la “Kuza Mti Tukutuze”.
Thamani ya shindano hilo ni TZS milioni 472 na lengo lake ni kuhakikisha miti itakayopandwa inakua na kuleta matokeo chanya. Washindi wake watangazwa mwezi Juni mwaka 2024 huku zawadi tatu za kwanza zikiwa ni pesa taslimu TZS milioni 50, 30 na 20.
Naye, Dkt. Mboya alisema, “Kupanda miti mipya milioni moja ni jambo kubwa katika mkoa wetu. Huu ni mchango muhimu katika harakati za kulikabili janga la athari za tabia nchi na ni wajibu wetu sisi wote na kama taifa kuziunga mkono taasisi kama NMB zinazoupa utunzaji mazingira kipaumbele ,”
Mbali na viongozi wa mkoa, wilaya na manispaa, zoezi la kupanda miti siku hiyo pia liliwashirikisha wananchi wa Kata ya Ifucha, maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, watumishi wa umma, wakereketwa wa mazingira na wanafunzi wa shule mbili za msingi katika kata hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇