LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 23, 2023

RAIS SAMIA ATIMIZA AHADI YAKE KWA MAWAKILI WA SERIKALI, AMKABIDHI AG 'LAPTOP' 150

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa komputa mpakato (Laptop) 150 kwa ajili ya mawakili wa Serikali ikiwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba mwaka jana.

Vifaa hivyo vya Tehama, vimekabidhiwa jana Jumatano Machi 22, 2023, kwa  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji  Dk. Eliezer  Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Moses Mpogole Kusiluka, kwa niaba ya Rais  Samia, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dodoma na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa  Mashtaka Sylvester  Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Boniphace  Luhende.

Akizungumza katika hafla ya hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Kusiluka amesema, ni matumaini ya Rais kuwa, vifaa hivyo vya tehama vitaboresha na kuongeza ufanisi wa Mawakili wa Serikali katika utekelezaji wa  majukumu yao.

“Tumekutana katika hafla hii fupilakini muhimu sana. Rais alitoa maelekezo tukutane ili nikukabidhi vifaa hivi vya Tehama ambayo aliridhia  wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali  uliofanyika Septemba 2022 hapa Dodoma.

Ni matarajio ya Rais kuwa vitendea kazi hivi vitatumika kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu  ya mawakili wa Serikali hasa kwa kuzingatia umuhimu wa matumizi ya tehama katika tasnia ya sheria”, akasema Katibu Mkuu  Kiongozi.

Katibu Mkuu kiongozi Kusiluka akaeleza zaidi kwa kusema “Sote tunafahamu Mhe. Rais  ametoa kipaumbele  katika kuboresha mifumo ya haki jinai na haki kwa ujumla, hivyo basi juhudi za Rais na serikali  kupitia msaada huu ni kuona ufanisi  wa mawakili wa serikali nao unaongezeka”.

Katibu Mkuu Kiongozi Kusiluka, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia Mawakili wa Serikali kadri  itakavyowezekana hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imejikita katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo inahitaji wataalamu wabobevu katika kila eneo wakiwamo Mawakili wa Serikali.

“ Serikali inathamini mchango wa Mawakili wa Serikali, ni matumaini ya Rais na ya kwangu kwamba, ninyi viongozi wa Taasisi mtaendelea kusaidia na kuhamasisha wataalamu wenu kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati” akasisitiza Katibu Mkuu Kiongozi.

Akizungumza baaada ya kukabidhiwa vifaa hivyo vya Tehama,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Feleshi, amesema Komputa  mpakato hizo zitaleta heshima na ufanisi zaidi  wa kazi kwa Mawakili wa Serikali.

“Kwa niaba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili  Mkuu wa Serikali, natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais, kwa kuridhia na kutupatia vifaa hivi vya tehama, ametuangalia  kwa jicho la umama na kwa kweli ni upendo wake wa dhati” akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akasema, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba 29 mwaka jana, ambao  Rais  alikuwa  mgeni rasmi na akazindua Chama cha Mawakili wa Serikali, alibainisha changamoto mbalimbali zikiwamo za uhaba wa vitenda kazi kwa maana ya Vifaa  vya Tehama kwa  mawakili wa Serikali

“Katika  Mkutano ule tulielezea changamoto mbalimbali  zikiwamo za miundombinu, upungufu wa  watumishi, lakini pia tukaelezea hili la vitendea kazi kwa maana ya vifaa vya tehema ili kwenda sanjari na maboresho yanayoendelea katika Tasnia ya Sheria.

Hata katika majadiliano ya migogoro baina ya Serikali na Wadau wetu, vikao vingi vinafanyika kwa njia ya  Tehema jambo ambalo Mawakili wetu wapo  nyuma kutokana na kutokuwa na vitenda kazi vya kisasa, vifaa hivi vitaleta heshima kubwa kwa mawakili wetu wa Serikali wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao” akasisitiza  Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali Dk. Feleshi,  akasema, vifaa hivyo vya Tehama si kwamba  vinahitajika kwa Mawakili wa Serikali peke yao bali hata  kwa Divisheni na Vitengo wezeshi  akitolewa  mfano wa Kurugenzi ya Utawala na Raslimali Watu,  Kurugenzi ya Mipango na Masijala.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi, tunafahamu mchakato huu umegharimu fedha na muda wa Mheshimiwa Rais na Serikali, sisi sote hapa ni wateule wa  Rais na ukisha kuwa mteule wa  Rais huna mambo yako, tunafuatilia na kusikiliza shughuli za Mheshimiwa Rais, niahidi kwamba tutatumia vifaa hivi  ili kwa pamoja na Serikali tuweze kuleta nafuu kwa Watanzania”, akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katibu Mkuu  Kiongozi Mhe. Dkt. Moses Kusiluka (kulia) akimkabidhi Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe.Jaji Dkt.  Eliezer  Feleshi  Komputa Mpakato 150 ambazo  Mhe. Rais Samia Suluhu  Hassan  aliridhia kwa ajili ya  Mawakili wa Serikali baada ya kuombwa na Mwanasheria Mkuu wa  Serikali  wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali  uliofanyika Septemba 2022 Mkoani  Dododma. 

Katibu Mkuu  Kiongozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka  akizungumza kabla ya kumkabidhi Mwanasheria Mkuu wa Serikali Komputa Mpakato150 ambazo zimetolewa na Mhe. Rais  kwa ajili ya matumizi ya Mawakili wa Serikali

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akitoa shukrani zake kwa Mhe. Rais baada ya kupokea  vifaa vya Tehama  kwaajili ya matumizi ya  Mawakili wa Serikali . Vifaa hivyo  viliombwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali  wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali  uliofanyika mwezi Septemba 2022 na mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungnao wa  Tanzania.

Mkurugenzi wa  Mashtaka Bw. Sylvester  Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali   Dkt. Boniphace Luhende nao walikuwepo  katika hafla hiyo ya makabidhiano ya  vifaa hivyo vya Tehama iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Dodoma. Vifaa hivyo vya Tehama  vitaganywa katika Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili  Mkuu wa Serikali.

Katibu Mkuu  Kiongozi Mhe Dkt. Moses  Kusiluka (kushoto), akiwa na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe Jaji. Dkt. Eliezer  Feleshi, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester   Mwakitalu, Wakili Mkuu wa  Serikali  Dkt. Boniphace Luhende na Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Dkt. Evaristo  Longopa wakiangalia  maboksi yenye vifaa vya Tehama ( komputa mpakato) ambavyo Rais aliridhia  kwaajli ya Mawakili wa Serikali.

 
Imeandaliwa na kutumwa kwetu na Kitengo  cha Mawasiliano, Ofisi ya AG.
22/03/2023

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages