Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, akizungumza katika katika kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), cha kujadili namna bora ya utekelezaji wa moangi wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, akizungumza katika katika kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), cha kujadili namna bora ya utekelezaji wa moangi wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru akiteta jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete baada ya kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), kilichojadili namna bora ya utekelezaji wa mpango wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, jijini Dodoma.
Kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), cha kujadili namna bora ya utekelezaji wa PPP pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru akimsikiliza Bi. Atal Agarwal kutoka Benki ya Dunia wakati wa kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), kilichojadili namna bora ya utekelezaji wa Mpango wa Ubia kati ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, jijini Dodoma.
Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru amesema kuwa Serikali inafanya majadiliano ya kimkakati na Benki ya Dunia (WB) namna ya kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, yaani PPP.
Alieleza hayo jijini Dodoma baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki hiyo Bw. Nathan Belete, ambapo walijadili namna bora ya utekelezaji wa sheria ya PPP pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Alisema majadiliano hayo ni utekelezaji wa msisitizo na maelekezo yanayotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa sasa ni wakati wa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.
Bw. Mafuru alisema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kila wakati kuwa pale ambapo Sekta Binafsi inaweza kufanya jambo fulani basi hakuna haja ya kutumia fedha za Serikali, lakini changamoto ilikuwa ni namna na mfumo ambao unaweza kusaidia miradi kufanyika kwa njia ya PPP.
“Wenzetu wa Benki ya Dunia wamekua mstari wa mbele katika kutoa fedha sio tu katika miradi ya kijamii, lakini sasa wanajielekeza zaidi kutoa fedha na misaada ya kitaalam kuhakikisha kwamba eneo hili la PPP sambamba na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara nchini yanafanikiwa”, alisema Bw. Mafuru.
Alisema kwa sasa Serikali imeanza majadiliano ya awamu ya pili na Benki ya Dunia kuhusu msaada ambao umejielekeza kwenye sekta za miundombinu na sekta zitakazoboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.
Aidha, alibainisha kuwa Sheria ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) inafanyiwa marekebisho ili iweze kuwa shindani, ambayo itaweza kuvutia mitaji ya Sekta Binafsi na hatimaye kiwezesha sekta hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi.
Alisema hatua hiyo itaweza kuipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti ili fedha ambazo zilipangwa kutumika kwenye miradi ambayo inaweza kufanywa na Sekta Binafsi zielekezwe kwenye sekta za kijamii ambazo haziwezi kuvutia Sekta Binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete alisema benki hiyo imeamua kujadiliana na Tanzania kuhusu namna bora ya utekelezaji wa miradi kwa njia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema majaliano na Serikali yalikuwa mazuri na anaamini kwamba makubaliano yao yataleta mabaliko katika mfumo wa utekelezaji wa PPP nchini na kuchochea maendeleo ya nchi.
Bw. Belete aliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika kutekeleza matarajio ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇