LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 20, 2023

WADAU WAPONGEZA KASI YA MAENDELEO KALIUA

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Jerry Daimon Mwaga akiongea na wadau, watumishi na watendaji wa halmashauri hiyo juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo. Picha na Allan Kitwe.

Na Allan Kitwe, 

Tabora HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora imepongezwa na wadau mbalimbali kwa mafanikio makubwa ya utekelezaji miradi ya maendeleo iliyopata katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na nishati ya umeme katika kipindi cha miaka 2. 

Wakiongea na gazeti hili baadhi ya wadau wakiwemo wanasiasa wakazi wa Wilaya hiyo wameeleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mtendaji Jerry Mwaga na Mwenyekiti wa halmashauri Jafael Lufungija. Walieleza kuwa juhudi, weledi na mshikamano mzuri wa Viongozi hao kwa kushirikiana na madiwani vimekuwa chachu ya maendeleo makubwa yanayoonekana sasa katika wilaya hiyo. 

Joseph Kagoma (65) mfanyabiashara mkazi wa kata ya Igagala alisema katika kipindi cha miaka 3 huduma za afya zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa sana kutokana na ujenzi wa zahanati za kutosha, vituo vya afya na hospitali ya wilaya.

Aliongeza kuwa mbali na ujenzi wa vituo vipya vya kutolea huduma hizo, miundombinu ya vituo vya zamani nayo imeboreshwa zaidi hali iliyopelekea wananchi kupata huduma hizo karibu zaidi na maeneo yao hivyo kilio chao. Mwalimu Mstaafu Mathew Kalugasha (75) alisema miundombinu ya shule nyingi katika halmashauri hiyo ilikuwa mibovu sana hali iliyopelekea watoto wengi kuacha shule na utoro kuwa mwingi zaidi, lakini sasa shule zote zimekuwa mpya. 

Alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Wataalamu na Watendaji wa vijiji na kata kwani kila mwaka wamekuwa wakitenga bajeti ya kuzifanyia maboresho shule zote kupitia fedha za ndani. 

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo aliyemaliza muda wake, Elias Kaseko, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea Mkurugenzi mchapa kazi na mwenye maono ya maendeleo, ambaye amebeba dhamana ya kweli. ‘Kaliua sasa inang’ara kwa ukusanyaji mapato, ufaulu mzuri wa wanafunzi, miundombinu bora ya afya na elimu, huduma bora za afya, barabara nzuri na mengine mengi, hakika ilani ya CCM imetekeleza kwa asilimia 100’, alisema.

Katibu wa CCM wilaya, Eliud Shemauya alieleza kuguswa na Ofisi ya Mkurugenzi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambao umepelekea miradi kukamilika kwa wakati na kutatuliwa kwa kero nyingi za wananchi. 

Alipongeza serikali kwa kuwapatia fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara ambayo imesimamiwa vizuri halmashauri na kukamilika kwa wakati. Aidha aliomba halmashauri hiyo kuongezewa watumishi wa sekta ya afya na elimu ili kupunguza uhaba uliopo kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali ya wilaya na baadhi ya shule.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages