LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 22, 2023

SERIKALI YAIPATIA TCU SH. BIL. 6.4 KUIMARISHA UTHIBITI UBORA, UHUISHAJI MITAALA


Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa a akieleza baadhi ya  mafanikio ya tume hiyo wakati wa mkutano na vyombo vya habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma Februari 22, 2023.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Seikali, Geron Msigwa  akifafanua mambo wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Zamaradi Kawawa akiongoza mkutano huo.
Mwandishi wa habari wa Azam TV, George Mbara akiuliza swali.
Baadhi ya wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.


PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA

Na Richard Mwaikenda, Dodoma

Serikali imeipatia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Sh. bil 6.4 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuishwa.

Hilo limebainishwa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa alipokuwa akieleza kuhusu mafanikio ya tume hiyo wakati wa mkutano na vyombo vya habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma Februari 22, 2023.

Profesa Kihampa mafanikio mengine kuwa ni kuendelea kuandaa na kuratibu mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa viongozi na wanataaluma wa vyuo vikuu kuhusiana na uendeshaji wa vyuo vikuu, utengenezaji mitaala inayozingatia ujuzi na inayoendana na soko, mbinu za ufundishaji kwa Wahadhiri ambao hawakusoma fani za ualimu, ulinganifu wa programu za masomo, uthibiti ubora na utengenezaji na utumiaji wa mifumo ya kompyuta.

Aidha, Prof. Kihampa amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2022, jumla ya viongozi na wanataaluma 575 wameshanufaika na mafunzo hayo ambayo yamelipiwa na Serikali kwa asilimia 100. Kutokana na hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali, vyuo vikuu vimeweza kuimarisha mifumo yake ya uthibithi ubora na uendeshaji wa mafunzo.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa fursa za masomo ya elimu ya juu na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini ambapo Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuongeza wigo wa fursa za masomo ya elimu ya juu kwa watanzania.

"Katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dkt. Samia madarakani, fursa mbalimbali za masomo zimeongezeka ikiwemo nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu katika programu za Shahada ya Kwanza zimeongezeka kutoka 157,770 mwaka 2020/21 hadi 172,168 mwaka 2022/23. Hili ni ongezeko la nafasi 14,398 sawa na asilimia 9.1,"amesema Prof. Kihampa.

Amesema kuwa programu za masomo ambazo zimeruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza zimeongezeka kutoka 686 mwaka 2020/21 hadi 757 mwaka 2022/2023 na kwamba wanaodahiliwa katika shahada ya kwanza wameongezeka kutoka 87,934 mwaka 2020/21 hadi 113,383 mwaka 2022/23 sawa na asilimia 28.9.

Idadi ya Wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu imeongezeka kutoka 259,266 mwaka 2020/21 hadi 295,919 mwaka 2021/22 sawa na asilimia 14.1. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka kwa mwaka wa masomo 2022/2023.


 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages