LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 12, 2023

RAIS MSTAAFU DK. KIKWETE AONGOZA KAMATI YA UANGALIZI YA SADC NCHINI LESOTHO

Na Mwandishi Maalumu
Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Panelof Elders, POE) leo ameongoza Ujumbe wa Kamati ya Uangalizi ya SADC inayofuatilia Utekelezaji wa Makubaliano ya Amani nchini Lesotho katika ziara nchini humo.

Ziara ya Kamati hiyo ya Uangalizi ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC katika Mkutano wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Kinshasha, DRC mwezi Agosti 2022 ambapo walilielekeza Baraza hilo la Wazee la SADC kufuatilia kwa karibu jitihada za usuluhishi wa migogoro inayoendelea kwa muda mrefu katika Falme za Lesotho na Eswatini.

Rais Mstaafu Kikwete ameongozana na Makamu wa Rais Mstaafu wa Mauritius, Paramasivum Vyapoory, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wazee amepata wasaa wa kukutana na Mtukufu Motlotlehi Letsie III, Mfalme wa Lesotho, viongozi wakuu wa Serikali ya Lesotho pamoja na wadau wengine muhimu katika mgogoro huo.

Kamati pia imepata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Lesotho ambaye ndiye Mkuu wa Serikali, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Haki, Sheria na Masuala ya Bunge, Spika wa Bunge, Makamu Rais wa Seneti, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kiongozi wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko, Viongozi wa Vyama vya Siasa vya Upinzani vilivyo Bungeni, Vyama vya Siasa vilivyo nje ya Bunge, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Askofu Mkuu wa Baraza la Kanisa la Kikristu nchini Lesotho pamoja na Mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza, Afrika Kusini na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa.

Katika mikutano yote iliyofanyika, Kamati hiyo imesikiliza kwa kina maoni ya wadau hao wote kuhusu namna bora zaidi ya kuweza kuendeleza kazi nzuri ambayo tayari imeshafanyika katika kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro uliopo nchini humo. Kamati hiyo inaripoti kwa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika) ambaye kwa sasa ni Hage Geingob, Rais wa Namibia.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakata Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Panel of Elders) akikutana  viongozi wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Lesotho alipoongoza ujumbe wa Kamati ya Uangalizi ya SADC inayofuatia makubaliano ya amani nchini humo kuanzia tarehe 08 hadi 11 Februari

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages